Tuesday, 12 July 2011

Walemavu wapewe kazi ya heshima na wawe wazalishaji wa mali za jamii



Jamii haina budi kutambua kuwa "walemavu wanawezeshwa kupata ajira ya heshima" ili waweze kujikimu kimaisha kama binadamu wengine.
Katika miaka ya hivi karibuni nchi mbalimbali zimepitisha sheria kwa lengo la kuhakikisha walemavu hawabaguliwi, bali wanasaidiwa kuinua maisha yao.
Baadhi ya walemavu wamepata ajira na kujiunga na jamii, lakini sehemu kubwa ya walemavu bado wanakabiliwa na matatizo ya kutoajiriwa na umaskini.
Kwa mujibu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), kuna walemavu milioni 650 duniani ambao ni moja kwa kumi ya idadi ya watu wote duniani, kati yao milioni 500 ni wafanyakazi.
Asilimia 80 ya walemavu wako katika nchi maskini kama vile Tanzania.
Watu hao wanaishi chini ya kiwango cha maisha kilichowekwa na Umoja wa Mataifa, walemavu ni watu wenye shida kubwa zaidi katika jamii ya watu wanyonge.
Kama hali hiyo haitabadilika, itakwamisha maendeleo ya jamii na pia itaathiri kutimiza kwa malengo ya milenia yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa ya kupunguza watu maskini kwa nusu ifikapo mwaka 2015.
Ripoti pia inasema umaskini wa walemavu unaondolewa kwa kuwapatia ajira. Pamoja na msaada wa jamii walemavu wanapaswa wajitatulie wenyewe matatizo yao kwa kufanya kazi. Ripoti inasema hali ambayo walemavu mamilioni kumi kadhaa wenye uwezo wa kufanya kazi hawapati ajira ni hasara kubwa kwa nguvu kazi za jamii. Kutokana na makadirio ya utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia, hasara zinazosababishwa kila mwaka na watu wasio na ajira katika uzalishaji mali zinafikia thamani ya dola za Kimarekani trilioni 1.37 hadi rilioni 1.94.
Kadhalika ripoti hiyo pia inasema, kazi ya walemavu inapaswa kuwa ya heshima, lakini hivi sasa ajira zao bado ni duni na zenye vipato vya chini, na wanaofanya kazi za kiteknolojia na zinazohitaji kutumia akili zaidi ni wachache sana. Hali hiyo inatokana na sababu nyingi, ikiwa ni pamoja na kuwa walemavu hawakupata elimu ya kutosha, hawana ufundi mkubwa, wanazuiliwa na sera za ajira; mazingira ya kazi, tatizo la usafiri, na ubaguzi kutoka kwenye jamii na kutoka kwa wafanyakazi wenzao.
Shirika la Kazi duniani linasema, tarehe 13 Desemba mwaka jana baraza kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha mkataba wenye maana ya kihistoria wa "Haki za Walemavu Duniani", mkataba huo ambao ni wa kwanza kabisa duniani kuhakikisha haki za walemavu umepitishwa na kusainiwa na nchi 80, hii ni nguvu ya kusukuma nchi mbalimbali zitunge sheria za kuhakikisha haki za walemavu na kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa. ILO inataka nchi zote zifanye juhudi kubwa zaidi ili kuondoa kabisa hali ya ubaguzi katika ajira kwa walemavu, ili wapate kazi zenye heshima na kuzalisha thamani nyingi zaidi ya kijamii.

No comments:

Post a Comment