Wednesday 6 July 2011

POSHO ZA WABUNGE ZIFUTWE: NI MZIGO KWA WANANCHI MASKINI





UFAFANUZI uliotolewa na waziri mkuu bungeni hivi karibuni ni kioja kitupu na ni kupotosha ukweli wa mambo.

Hivi ni kweli kuwa wabunge wanalipwa ili nao wakawape wapira kura wao fedha, watawapa wangapi?

Nadhani waziri mkuu hakusema ukweli, kwani ulimi uliteleza.

Hawa jamaa akina Kabwe Zitto siyo kwamba wanataka posho zote zifutwe hapana, ni posho moja tu; tena ndogo sana ambayo ni posho ya kukaa kwenye kiti tu(sitting allowance) ambayo ni shilingi 70,000/- kwa siku kwa kila mbunge na kila mkurugenzi, mkuu wa idara, katibu mkuu na maofisa wengine wanapokaa kwenye viti vyao kwa ajili ya kikao cha kikazi ambacho ni sehemu yao ya kazi za kawaida.

Ukweli wa mchanganuo na mishahara ya wabunge na posho zao ni kama ifuatavyo:

Tangu Novemba, 2010 hadi Novemba, 2015 bunge lingine litakapochaguliwa; kila mbunge atakuwa akilipwamshahara wa mwezi 7,500,000/-; posho ya diesel lita 700 kwa mwezi ili aweze kutembelea jimbo lake vizuri na kila lita imepigiwa mahesabu ya 2,500/-

Jumla ni 1,750,000/- kwa mwezi; posho ya dereva kila mwezi 400,000/-

Posho ya katibu wa mbunge kila mwezi 400,000/-; posho ya matengenezo ya gari la mbunge ni 1,000,000/- kwa kila mwezi na posho ya vikao vya kamati, bunge, semina na vikao vingine kwa mwezi ni wastani wa siku 15 kila mwezi, kila siku ni 80,000 (posho ya kujikimu) na 70,000/- (posho ya kukaa kitini (sitting allowance), jumla posho ya vikao, semina nk ni 150,000/- kwa siku ambayo kwa siku 15 ni Shilingi 2,250,000/-.

Ukijumlisha mshahara na marupurupu mengine, yaani mshahara na posho zote hizo maana wengi wao hata zile za madereva na makatibu wao huzichukua wao wenyewe; utakuta mbunge wa Tanzania anakunja milioni 13 kwa mwezi mmoja.

Ukiondoa kodi kwenye mshahara ya 525,000/- anabakiwa na takribani 12,775,000/- anazoipelekea familia yake nyumbani kwake.

Hapo umeshaondoa fursa zingine ama kusafiri nje ya nchi ambapo hulipwa 800,000/- kwa siku.

Posho ambayo CHADEMA wanaikataa ni ile posho ya kukaa tu kwenye kiti 70,000/- kwa siku.

Kwa maana hiyo, posho zenye mantiki wanazikubali; posho hiyo ikiondolewa inapunguza malipo kwa mbunge kwa mwezi kwa 1,050,000/- tu; yaani badala ya kulipwa 12,775,000/-, posho hiyo ikiondoloewa kila mbunge atalipwa 11,725,000/- kwa mwezi.

Faida kwa nchi inayoweza kupatikana kutokana na punguzo hilo ni kuokoa 4,309,200,000/- kwa mwaka, ambazo zinaweza kuingizwa kwenye bajeti ya maendeleo.

Fedha hizo zinaweza kuchimba visima vya maji 287 vyenye uwezo wa kuhudumia watu wapatao 100,000 kwa mwaka.

Kwa miaka mitano ina maana watu 500,000 watafaidika na punguzo hilo.

Je, Watanzania wengine mna maoni gani? Ukiondoa posho zote za kukaa tu kwenye kiti serikalini na mashirika ya umma (total sitting allowances), unaweza kuokoa zaidi ya 90,000,000,000/-!

No comments:

Post a Comment