Kuanzia tarehe 28 Juni hadi 1 Julai 2011, kwa muda wa siku nne, Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) utasambaza wafanyakazi wake katika kanda tano nchini kukutana na wanaharakati wa ngazi ya jamii kwaajili ya warsha ya kujengeana uwezo na nguvu za pamoja katika kujenga tapo la mabadiliko katika jamii, ambalo litachangia kuwepo kwa jamii yenye mabadiliko, yenye kutambua na kuthamini masuala ya jinsia, demokrasia, haki za binadamu na haki za kijamii.
Mafunzo haya yatalenga kujenga nguvu za pamoja katika kuendeleza kampeni ya haki ya uchumi katika ngazi ya jamii kwa kuongeza uelewa wa maana ya ‘Haki ya Uchumi: Rasilimali Ziwanufaishe Wanawake Walioko Pembezoni’ kwa mtazamo wao wenyewe kwa kuzingatia mjadala mpana wa uundaji wa Katiba mpya.
Mikoa ambayo imepata fursa hiyo kwa kipindi hiki ni Kanda ya Kaskazini Mkoa wa Kilimanjaro, Kanda ya Mashariki Mkoa wa Morogoro, Kanda ya Kati ni Mkoa wa Dodoma, Kanda ya Ziwa ni Mkoa wa Shinyanga na nyanda za Juu Kusini ni mkoa wa Ruvuma. Baada ya warsha za wanaharakati kutafuatiwa na mafunzo ya waandishi wa habari namna ya kuandika habari za kijinsia katika mikoa ya Ruvuma na Shinyanga.
Katika mafunzo hayo, kutakuwa na timu ya watu wawili kutoka TGNP na mmoja kutoka katika kanda husika. Zoezi hili muhimu litaendeshwa kwa mbinu za kiraghbishi ili kuwapa wananchi nafasi ya kujadiliana zaidi, kuibua changamoto na fursa za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni walizonazo na jinsi wanavyoshirikiana kuzitatua na kama hazitatuliwi ni hatua gani wanachukua kuzitatua. Mwishowe wataweka mikakati madhubuti kwa hatua zaidi za utekelezaji na tathimini.
Pamoja na hayo, TGNP itatumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi juu ya umuhimu wa ushiriki wao katika mchakato mzima wa kuandika katiba mpya na nafasi ya mwanamke katika mchakato huu. Kadhalika TGNP itaelezea kwa kina juu ya Tamasha kubwa la Jinsia litakalofanyika jijini Dar es salaam tarehe 13-16, Septemba, 2011, namna watakavyoweza kushiriki.
Hiyo ni kazi nzuri ya kupongezwa sana
ReplyDelete