Thursday 15 September 2011

KATIBA MPYA NI LAZIMA , TENA SASA

JAJI Mstaafu, George Liundi amesema wakati umefika kwa watanzania kuandika Katiba mpya kukidhi changamoto za ardhi, nguvu kazi na maisha endelevu zinawazowakabili wananchi.
Amesema katiba ya sasa ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo imeandikwa mwaka 1977 imepitwa na wakati na kwamba kinachotakiwa ni wananchi nchi nzima kuunganisha nguvu zao katika harakati za kuhakikisha taifa linapata katiba itakayowezesha wananchi kuendesha maisha yao.
“Hata mimi ambaye ndiye niliyeandika katiba hii naona imepitwa na wakati tunahitaji kuandika katiba mpya itakayokidhi mahitaji ya wananchi kwa miaka 50 ijayo,” alisema Jaji Liundi.
Jaji Liundi alisema hayo jana (Leo), katika warsha ya  “Mapambano kuhusu upatikanaji wa katiba zenye maslahi ya wananchi Afrika” kwenye Tamasha la Kumi la Jinsia linaloendelea kufanyika katika viwanja vya Mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP), Mabibo, jijini Dar es salaam.
Jaji Liundi alitoa ushauri huo baada ya kusikiliza visa mkasa vilivyotolewa na wananchi waliozungumza katika warsha hiyo kutoka Manyara, Kilimanyaro, Arusha, Morogoro, Mbeya, Mara, Dar es salaam, Ruvuma, Pwani na Pemba.
Watoa visa mkasa hao hao walieleza matatizo yanayowakabili wananchi kutokana na uwekezaji kwenye ardhi.
Mmoja wa watoa visa mkasa hao, kutoka kijiji cha Mkwangwelo, Morogoro alieleza kwamba mwekezaji mzungu wa KPL, katika kuendesha shughuli zake kwenye ardhi anatumia helkopta kunyunyizia sumu ya  kuua majani kwenye ardhi aliyopewa, ambayo huathiri mashamba ya watu wengine na kuangamiza mazao ya chakula kama mpunga.
“Wananchi wanakabiliwa na janga la njaa kutokana na mpunga wao kuangamizwa na hiyo sumu hiyo,” alisema Clavery Mwakinyonge kwenye warsha hiyo.
Mshiriki mwingine, kutoka Manyara Hanang, Martha Laurent Sumaye alisema mwekezaji aliyepewa kulima kwenye ziwa Basutu amekuwa akiwanyanyasa wananchi wa eneo hilo.
Alisema mwekezaji huyo anapolima vitunguu amekuwa akiziba maeneo yote, zikiwemo nja za wananchi kwenda kufuata mahitaji muhimu kama maji, kuni sambamba na njia ambazo mifugo ilikuwa ikipita.
Alisema kutokana na hali hiyo kumezuka mapambano kati ya wananchi na mwekezaji huyo na kwa miezi minne sasa wanawake wamekuwa wakiishi porini kwani wanapodai haki yao ya kupata njia wamekuwa wakinyanyaswa na kufanyika vitendo vya ukatili.
Mzungumzaji mwingine kutoka Nyamongo, Bani Moto alisema mgodi wa Mwekezaji wa mgodi wa Goldmine unasababisha  sumu kuingia kwenye mto  na wananchi wengi na mifugo wanaotumia maji hayo wa imeathirika.
Kabla ya kutoa visa mkasa hivyo, Kiongozi wa Mtandao wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba alikuwa amewaeleza washiriki wa warsha mambo mazuri ya;liyopo kwenye katiba ya sasa ambayo yanawalinda wananchi ambayo yanahitaji kuendelea kwenye katiba mpya.
Alisema kwa mujibu wa katiba ya sasa, ibara ya 8,1(a), wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba.
Hata hivyo alisema katiba hiyo inawaondolewa wananchi madaraka kwa sababu inampa mkuu wa nchi mamlaka ya mwisho kuhusu umiliki wa ardhi.
Wanawarsha hao wamependekeza kuwa katika katiba mpya, mamlaka kuhusu ardhi yawe mikononi mwa wananchi wenyewe ili kuepusha viongozi wa juu kuwapa wawekezaji ardhi ya wananchi huku wananchi wakinyanyaswa na wawekezaji na kukosa ardhi yenye rutuba kuendesha maisha yao.
Mwenyekiti wa kijiji cha Arash, Loliondo, Ngorongoro, Kiaro Orminis alisema kuwa kutoka mgongano kwamba viongozi wa juu ndio wenye mamlaka kuhusu ardhi, viongozi wa juu wamekuwa wakiwalazimisha viongozi wa chini kufanya vitu ambavyo vinaenda kinyume na maslahi ya wananchi

No comments:

Post a Comment