Monday, 5 September 2011

Hotuba ya Raisi Jakaya Kikwete kwa Waislamu huko Dodoma





HOTUBA YA MH. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE BARAZA LA EID-EL-FITR, DODOMA, TAREHE 30 AGOSTI, 2011 
Mheshimiwa Sheikh Issa bin Shaaban Simba, Sheikh Mkuu
na Mufti wa Tanzania,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya BAKWATA;
Wajumbe wa Baraza la Ulamaa;
Waheshimiwa Masheikh na Viongozi wa BAKWATA;
Waheshimiwa Viongozi wa Dini wa
Madhehebu Mbalimbali;
Viongozi Wenzangu wa Chama na Serikali;
Ndugu Wananchi; Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana;

Assalaam Ellaykum Warahmattullah Taallah Wabarakatuh!

Eid-Mubarak!!

Nakushukuru sana Mheshimiwa Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika siku hii adhimu ya kusherehekea kumalizika kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Naungana na nawe na Katibu Mkuu wa BAKWATA Sheikh Suleiman Saidi Lolila kumshukuru Allah Subhana Wataalah kwa kutuwezesha kufunga na kutimiza moja ya nguzo tano za Uislamu. Inshaalah tuzidi kumuomba Mola wetu aendelee kutujaalia uhai na uzima ili tuweze kufunga Ramadhani ijayo na za miaka mingi ijayo.

Mheshimiwa Mufti wa Tanzania;

Naungana nawe pia, kuwapongeza Waislamu wote nchini na duniani kwa kumaliza salama ibada ya swaumu kwa mwaka huu. Inshaalah tuombe kwa Mwenyezi Mungu sote tuwe miongoni mwa wale ambao funga zao zitakuwa zimekubaliwa. Aidha, tuombe tuwe miongoni mwa waja wake ambao toba zao zimetakabiliwa na kusamehewa madhambi yao na adhabu ya moto.

Napenda nami nijumuike nawe pamoja na , Katibu Mkuu wa BAKWATA na Masheikh wote nchini kuwaomba na kuwasihi Waislamu wote nchini kwamba, ucha Mungu tuliouonyesha katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan usiwe umeisha jana bada ya kuandama kwa mwezi. Badala yake, hauna budi uwe endelevu, kwa maana ya sisi kuendelea kutenda mema na kuepuka kutenda dhambi na mambo yanayomchukiza Mwenyezi Mungu. Katu ucha Mungu siyo kwenye kipindi cha Mwezi mtukufu peke yake.

Risala 

Mheshimiwa Mufti;

Nawashukuru sana kwa risala yenu iliyowasilishwa vizuri na Katibu Mkuu wa BAKWATA. Yote mliyosema kuhusu Serikali, nchi yetu, Waislamu na Watanzania kwa jumla nimeyasikia na kuyaelewa. Napenda kuanza kwa kusema kuwa Serikali inaunga mkono na inapenda sana kuwa na uhusiano na ushirikiano wa karibu na mashirika, viongozi na waumini wa dini zote nchini bila ya kubagua wala kupendelea.

Bila ya shaka mtakubaliana nami kuwa maneno haya niyasemayo leo si mageni kwako na masikioni mwa Watanzania. Nimeshayasema mara kadhaa siku za nyuma. Tena haya ni maneno ya dhati na wala siyo ya kuwapaka mafuta kwa mgongo wa chupa kama msemo wa Kiswahili usemavyo.

Mheshimiwa Mufti;

Serikali ina msimamo huo kwa sababu tunatambua na kuthamini sana nafasi na mchango wa dini na mashirika ya dini katika maendeleo na ustawi wa jamii na nchi yetu kwa ujumla. Serikali inaunga mkono mashirika ya dini katika shughuli zao kwa sababu ya manufaa ya dhahiri ya shughuli hizo kwa taifa letu. Mashirika ya dini yamekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Serikali kuwapatia wananchi wa Tanzania huduma muhimu za elimu, afya, maji n.k. Bila ya ushirikiano, upatikanaji wa huduma hizo kwa baadhi ya maeneo ungekuwa tofauti sana. Serikali kwa upande wake imekuwa inafanya kazi ya kusaidia mashirika ya dini yaweze kutoa huduma hizo kwa wananchi.

Napenda kuwahakikishia kuwa hakuna kitu cho chote ambacho Serikali itatoa kwa dini moja ambacho dini nyingine itanyimwa. Kwa kweli mbele ya Serikali dini zote zina haki sawa. Kama hujaomba usimlaumu aliyeomba akapewa au aliyempa. Kama yupo anayeamini anazo sifa kama mwenzake aliyepewa aombe naamini atapewa. Iwapo itafanyika vinginevyo dai haki yako kwa mamlaka zinazohusika.

Mheshimiwa Mufti, Ndugu Zangu Waislamu;

Maelezo yangu haya yanafanana na hoja zenu katika Risala yenu kuhusu Itifaki ya Maridhiano ya 1992 baina ya Serikali na TEC na CCT. Nafurahi kwamba na nyie mmeamua kuleta maombi, yaleteni yatashughulikiwa ipasavyo.

Mheshimiwa Mufti; Ndugu Zangu Waislamu; Watanzania Wenzangu Wote;

Sababu ya pili inayoifanya Serikali kuunga mkono madhehabu ya dini katika shughuli zao ni kazi kubwa yaifanyayo ya kuwalea Watanzania kuwa wacha Mungu. Sisi tunaamini kuwa kama madhehebu yatafanikiwa kwa hili nchi yetu itakuwa mahali pazuri sana pa kuishi. Wacha Mungu ni watu wema, hawatendi maovu, waaminifu, waadilifu, hawaombi, hawatoi wala kupokea rushwa. Wacha-Mungu ni watu wenye upendo kwa watu wote na daima hupenda amani, usalama na utulivu. Kwa sababu hiyo mambo mengi maovu katika jamii na Serikali yatapungua, watu watahudumiwa ipasavyo na hivyo kuvipunguzia vyombo vya dola kazi ya kupambana na uovu na uhalifu.

Uhuru wa Kuabudu 

Sababu ya tatu, Mheshimiwa Mufti, ni kuwa uhuru wa kuabudu unatambuliwa kuwa moja ya haki za msingi za raia wa Tanzania katika Katiba ya nchi na unalindwa kisheria. Watanzania wako huru kufuata na kuabudu dini yoyote waipendayo au kutokukufuata dini yoyote. Tanzania haina dini ya taifa au ya Serikali ambayo watu wote lazima waifuate. Aidha, hairuhusiwi kisheria kubeza au kudharau dini au imani ya mtu mwingine na hata nyumba za ibada. Imefanywa hivyo makusudi kwa nia ya kulinda uhuru wa watu kuabudu na kudumisha amani katika jamii na nchini. Naamini kama ingekuwa kinyume chake amani ingeweza kuvunjika.
Mheshimiwa Mufti, Waheshimiwa Masheikh na Watanzania Wenzangu;

Inasikitisha kusikia kuwa wapo viongozi na waumini wa dini zetu nchini wakipita huku na huko na wakati mwingine wakitumia nyumba za ibada kuhubiri kejeli dhidi ya dini nyingine. Kukashifiana hujenga chuki na uhasama baina ya waumini wa dini mbalimbali na kuhatarisha amani na usalama. Hivi viongozi wangu wa dini, hamuwezi kueneza imani ya dini zenu bila kukashifu dini ya wenzenu. Kama kweli wewe ni kiongozi wa dini unaetambua wajibu wako ipasavyo, huwezi kufanya hivyo na wala huhitaji kukumbushwa na Polisi kutokufanya hivyo. Tafadhali acheni na mamlaka husika acheni ulegevu kusimamia sheria. Ajizi yenu inaweza kuleta maafa katika taifa. Timizeni wajibu wenu ipasavyo bila woga wala kuonea au kupendelea.

Pamoja na hayo ni vyema viongozi wa dini zote na madhehebu yote mkafufua na kuendeleza utaratibu mzuri uliokuwepo siku za nyuma wa mawasiliano baina ya dini mbalimbali. Itasaidia sana kuzungumzia masuala ya namna hii na hata la uadui mlilolitaja katika Risala yenu. Nguvu ya dola peke yake si jawabu.

Hoja za Risala 

Mheshimiwa Mufti; Ndugu Zangu Waislamu,

Katika risala yenu mmezungumza mambo kadhaa mengine na kutoa ushauri mzuri ambao napenda kuwahakikisha kuwa tutaufanyia kazi. Hata hivyo, niruhusuni niyazungumzie au kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya mambo.

Mahujaji 

Mheshimiwa Mufti,

Napenda kukupongeza wewe na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa kazi kubwa na nzuri muifanyayo kuhusu upelekaji wa mahujaji Makka na Madina kila mwaka. Ni kweli kabisa kwamba BAKWATA inayo rekodi nzuri ya kuwasafirisha, kuwahudumia na kuwarejesha salama nyumbani mahujaji. Napenda kuwatia moyo kuwa muendelee kufanya vizuri zaidi mwaka hadi mwaka ili BAKWATA iwe chaguo la hiari la Waislamu wanaotaka kwenda kutimiza ibada ya Hija.

Pamoja na hayo, zipo taarifa za baadhi ya taasisi zinazoshughulikia upelekaji wa mahujaji kutokufanya vizuri. Matokeo yake mahujaji wamekuwa hawahudumiwi ipasavyo na safari ya Hija hugeuka kuwa adha badala ya kuwa furaha shangwe. Je, hamuoni umuhimu wa jambo hili kulitengenezea vigezo fulani ambavyo kila taasisi haina budi kuvizingatia katika usafirishaji, huduma na urejeshaji nyumbani wa mahujaji? Pia ingekuwa bora mkatengeneza utaratibu wa ushirikiano baina ya taasisi zote. Kufanya hivyo kunaweza kusaidia kunyoosha mambo pale yanapokuwa hayaendi vizuri. Inawezekana pia kwamba kupitia ushirikiano huo mnaweza kuandaa usafiri wa pamoja na huduma za pamoja kwa mahujaji wenu wawapo Makka na Madina na hivyo kupunguza gharama.

Ushirikishwaji Masuala ya Kitaifa 

Mheshimiwa Mufti;

Tumeipokea rai yenu ya kutaka Serikali iyatambue na kuyashirikisha mashirika ya dini kwenye mambo muhimu yahusuyo maslahi ya taifa kabla ya kutekelezwa. Rai hiyo ni njema na tutaizingatia. Hata hivyo, napenda kuwahakikishia viongozi wa dini zote na waumini wao kuwa hiyo ndiyo sera na utaratibu wa Serikali kwa miaka mingi na haujabadilika. Kama itatokea kutofanyika ni upungufu wa bahati mbaya au wahusika Serikalini ni wageni au wazembe.

Kwa suala hili la mchakato wa Katiba mpya nilikwishaeleza kuwa viongozi wa dini watashirikishwa katika hatua zote muhimu tangu kutoa maoni kuhusu masuala ya kuunda Tume, kwenye Tume yenyewe, mjadala, Bunge la Katiba na katika kura ya maoni.

Mheshimiwa Mufti;

Pamoja na ushirikishwaji huo napenda kurudia rai au tahadhari niliyoitoa wakati wa mkutano wangu na Maaskofu walio Wajumbe wa Jukwaa la Wakristo Tanzania tarehe 22 Julai, 2011 jijini Dar es Salaam. Niliomba tujitahidi kuhakikisha kuwa mjadala wa Katiba haugeuki kuwa mdahalo au malumbano kati ya Wakristo na Waislamu kuingiza maslahi ya dini zao katika Katiba. Tukiufikisha hapo, kutatokea mivutano ambayo ni migumu kuipatia majibu na kuna hatari ya Katiba mpya kushindikana kupatikana au kuchelewa sana na hata amani kuvunjika. Inaweza kuwa ndiyo mwanzo wa umoja wa taifa letu tulioujenga kwa takriban nusu karne kuvurugika kwa namna ambayo itakuwa vigumu kuujenga tena. Napenda kuona wote wanapata fursa ya kushiriki kwa lengo la kuhakikisha kuwa Tanzania inabaki kuwa nchi ya watu wa dini zote, wenye umoja miongoni mwao. Tanzania inaendelea kuwa haina dini ingawaje raia wana dini na uhuru wa kuabudu umehakikishwa na kulindwa ndani ya Katiba kwa mujibu wa na Sheria za nchi. Hali linawezekana kama viongozi wa dini tutataka kwa dhati iwe hivyo.

Shule za Taasisi za Kiislamu 

Mheshimiwa Mufti; Ndugu Zangu Waislamu na Watanzania Wenzangu;

Nimesikia maelezo na maombi yenu kuhusu shule zilizokuwa zinamilikiwa na taasisi za Kiislamu zilizotaifishwa na Serikali baada ya Uhuru. Ni kweli kwamba mara baada ya Uhuru shule zote za msingi, sekondari na vyuo vilivyokuwa vinamilikiwa na mashirika ya dini na jumuiya za kijamii zilitaifishwa. Ni kweli pia chache kati ya hizo zilirejeshwa kwa wamiliki wa awali katika miaka ya 1990. Ni kweli vile vile, kwamba mashirika ya dini ikiwemo BAKWATA na jumuiya za kijamii zimekuwa zikiomba kurudishiwa shule hizo lakini Serikali haijayakubali maombi hayo.

Mheshimiwa Mufti; Waheshimiwa Masheikh;

Katika mkutano wangu wa tarehe 22 Julai, 2011 na Jukwaa la Wakristo suala hili lilijitokeza na nililitolea ufafanuzi ambao napenda nirudie kuueleza hapa leo. Baba wa Taifa na Rais wa Kwanza wa nchi yetu, Mwalimu Julius Nyerere aliamua kutaifisha shule zote za mashirika ya dini na jumuiya za kijamii hasa za Wahindi na Wazungu kwa lengo la kutoa fursa sawa ya kupata elimu kwa watoto wa dini zote, wasiokuwa na dini na wa rangi zote bila kubaguliwa.

Kutokana na uamuzi ule hakuna mtoto aliyebaguliwa kupata elimu kwa sababu ya rangi yake au dini yake. Hata wale waliotoka kwenye jamii ambazo kwa dini zao au rangi zao hawakuwa na shule kabisa au walikuwa nazo kidogo waliweza kupata nafasi, bora tu wawe na sifa stahiki hasa za kufaulu mitihani na nyinginezo. Lakini si hivyo tu, ili kujenga usawa kwa upande wa sekondari Mwalimu alikwenda mbali zaidi. Serikali iligawa sawia nafasi za kwenda sekondari kwa mikoa na wilaya nchini na siyo tu kufuata kigezo cha mtu kufaulu mitihani.

Mheshimiwa Mufti;

Baada ya kutaifisha shule hizo, ukiacha shule za msingi zilizojengwa karibu kila kijiji, Serikali haikuwekeza sana katika ujenzi wa shule mpya za sekondari. Matokeo yake wakati ule katika mikoa yetu, ukizungumzia shule za sekondari za Serikali, kwa kweli nyingi, kama siyo zote, ni hizi zilizotaifishwa kwani Wakoloni hawakuacha shule nyingi na Serikali haikujenga nyingi mpya. Kwa kweli uwekezaji uliongezeka kwa wingi sana kwa shule za sekondari za Serikali katika Awamu ya Nne kwa ujenzi wa Sekondari za Kata.

Kwa kutambua ukweli kwamba shule za Serikali ni kidogo hata baada ya Serikali kutiliana saini Itifaki ya Makubaliano (MoU) na TEC na CCT mwaka 1992, kasi ya kurejesha shule ilikuwa ndogo sana na baadae ikasimama kabisa. Kilichosimamisha ni ule ukweli kwamba zingerudishwa zote Serikali ingejikuta kama vile haina shule za sekondari na badala yake shule zingekuwa mikononi mwa makanisa. Kitendo hicho kingezua manung’uniko na mgogoro katika jamii hasa baada ya zaidi ya miaka mingi shule hizo kuwa mali ya Serikali. Kwa ajili hiyo, pamoja na nia njema iliyokuwepo ya kuziboresha na kuziendeleza uamuzi huo ulikuwa mgumu kutekelezeka. Serikali ikajipa dhima ya kuziboresha na kuziendeleza.

Mheshimiwa Mufti; Viongozi wa Dini Zote;

Ushauri na maombi yetu kwa BAKWATA na mashirika mengine ya dini na jumuia zilizokuwa na shule wafikirie kuwekeza katika ujenzi wa shule na vyuo vipya badala ya kuendelea kudai shule zao za zamani. Ahadi kubwa ya Serikali inayotoa kwenu ni kuwa hazitataifishwa tena.

Dawa za Kulevya 

Mheshimiwa Mufti;

Kuhusu dawa za kulevya, sina budi kuwashukuru kwa msimamo wenu wa kutambua kuwepo tatizo na utayari wenu wa kushirikiana na Serikali katika mapambano haya. Msimamo huo unanipa faraja kwani kwa kweli tatizo ni kubwa sana. Sisi katika Serikali tumejipanga vizuri na tumeongeza sana nguvu ya kupambana na uovu huu. Tunapata mafanikio lakini kazi iliyo mbele yetu ni kubwa sana inayohitaji ushirikiano wa jamii nzima wakiwemo viongozi wa dini na waumini wao. Na huo ndiyo ujumbe wangu wa msingi nilioutoa Mwanza tarehe 29 Mei, 2011 wakati wa kuwekwa Wakfu Askofu Albert Jella Randa wa Kanisa la Mennonite na Mbinga tarehe 5 Juni, 2011 wakati wa kuwekwa Wakfu Askofu John C. Ndimbo wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga.
Bahati mbaya sana nilipoelezea masikitiko yangu kwamba hata baadhi ya watumishi wa Mungu wanajihusisha na biashara hiyo, imeeleweka ndiyo sivyo na kutafsiriwa isivyo. Ni kweli kama walivyoeleza vyema watu wanaoshughulikia tatizo hili, kwamba miongoni mwa waliokamatwa na kufikishwa Mahakamani wamo watumishi wa Mungu wa wa ngazi mbalimbali wa dini zetu zote. Hakuna Askofu wala Sheikh mzito.
Napenda kuwahakikishia kuwa mimi nitakuwa mtu wa mwisho au kutoa maneno ya kejeli kwa kuwashutumu watumishi wa Mungu. Kwanza sina sababu ya kufanya hivyo, lakini pia ninawaheshimu sana. Hata hivyo, nawiwa na wajibu kupeana taarifa na kutahadharishana na kuomba tushirikiane pale ukweli unapoonekana.
Nirudie kuwaomba viongozi wa dini zote tushirikiane na tusaidiane katika mapambano haya ambayo ni yetu sote. Ni jambo lenye maslahi mapana kwa taifa letu, leo na hasa kesho na kesho kutwa kwani walengwa na waathirika wakubwa wa dawa za kulevya ni watoto na vijana wetu ambao ndiyo warithi wetu na taifa la kesho.

Mahakama ya Kadhi 

Mheshimiwa Mufti;

Kuhusu mchakato wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi, nimeyasikia maoni yenu kwamba kumekuwa na kulegalega kwa upande wa Serikali jambo linalowafanya muingiwe na wasiwasi kuhusu nia njema ya Serikali katika mchakato huu. Napenda kuwatoa hofu kuwa hakuna kulegalega wala kubadilika kwa dhamira ya Serikali. Msimamo wa Serikali upo pale pale. Huu ni uamuzi uliofanywa na Chama chetu na Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya uongozi wa Rais Benjamin Mkapa wa kutaka kulitafutia ufumbuzi suala la Mahakama ya Kadhi na kuachiwa Serikali ya Awamu ya Nne kutekeleza.

Na sisi katika kufuatilia utekelezaji wa jambo hili tulikabidhi Tume ya Kurekebisha Sheria kuishauri Serikali. Ushauri wa Tume hiyo ulikuwa kwamba Serikali haiwezi kuunda Mahakama ya kushughulikia masuala ya kidini ya dini fulani. Jambo hilo liachiwe Waislamu wenyewe kufanya.
Serikali imekubali ushauri huo na ndipo mchakato ukaanza na tukaunda Kamati ya pamoja iliyojumuisha Serikali na BAKWATA. Nia ya Serikali ni kujihakikishia kuwa hicho kitakachoundwa hakiendi nje ya masuala ya kidini yaani ndoa, takala, mirathi na wakfu kwa mujibu wa dini ya Kiislamu. Katu si Mahakama ya kushughulikia masuala ya jinai au madai. Haitajihusisha na masuala ya wizi na kutoa adhabu kama vile za kukatwa mikono. Haitahusika na kesi za fumanizi na hivyo kutoa hukumu ya kuuawa mkosaji kwa kupigwa mawe. La hasha !! Narudia kuwa mamlaka yake yatahusu ndoa, takala, mirathi na wakfu. Isitoshe Muislamu hatazuiliwa kuamua kutumia sheria za nchi kwa masuala hayo akipenda kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mufti, Waheshimiwa Masheikh, Ndugu Zangu Waislamu;

Napenda kuwatoa hofu pia kwamba hakuna mkono wa mtu wapo mnadhania hivyo. Maana, tunajuana. Si ajabu kuna hisia kuwa huenda Kanisa limeingilia kati kuzuia au kuchelewesha. Siyo hivyo hata kidogo. Tarehe 22 Julai, 2011 nilipoalikwa kuzungumza na Maaskofu katika kikao chao cha Jukwaa la Wakristo katika risala yao kwangu kuhusu suala la Mahakama ya Kadhi walitoa ushauri ufuatao kuwa:
“Kuanzisha Mahakama ya Kadhi nchini na jambo zuri linalowahusu Waislamu. Kwa kuwa ni jambo la kidini waachiwe Waislamu wenyewe walifanye ndani ya Uislamu, pasipo kutumia hazina ya Serikali ambayo ni fedha ya walipa kodi wote nchini”

Hiyo ni nukuu kutoka ibara ya 6 ya Risala yao kuhusu Uhuru wa Kuabudu na dhana ya Udini.
Katika maelezo yangu kwao, niliwahakikishia kuwa mawazo yao yanawiana na yale ya Serikali kama ilivyoshauriwa na Tume ya Kurekebisha Sheria ambayo Mwenyekiti wake ni Profesa Ibrahim Juma. Mahakama hii itaundwa na Waislamu wenyewe ndani ya Uislamu wao na wataiendesha wenyewe na haitagharamiwa na Serikali.

Sheria ya Ndoa 

Mheshimiwa Mufti;

Ni kweli kwamba Serikali inao mpango wa kupeleka Bungeni Muswada wa Sheria wa kurekebisha Sheria ya Ndoa ya sasa. Napenda kuwahakikishia kwamba Serikali inatambua nafasi ya dini katika masuala ya ndoa na mirathi. Si nia ya Serikali kuanzisha ugomvi na madhehebu ya dini kuhusu suala hili na lingine lolote. Bahati nzuri taratibu za kutunga sheria ni taratibu zilizo wazi. Hazina usiri kwa upande wa maandishi na nyaraka wala hauna kificho katika kuzizungumzia. Miswada huchapishwa katika Gazeti la Serikali kwa kila mtu kusoma. Pia kuna utaratibu wa kushirikisha wadau kutoa maoni yao kabla ya muswada kuwasilishwa na kujadiliwa Bungeni.
Naomba nishauri kuwa Muswada utakapochapishwa katika Gazeti la Serikali muusome na mhakikishe kuwa mnaandaa vyema maoni yenu kuhusu vipengele mbalimbali vya Muswada. Kisha hakikisheni mnashiriki katika mikutano ya wadau kuwasilisha maoni yenu hasa katika maeneo mnayoona yana migongano na vitabu vitakatifu. Serikali yenu ni sikivu, naamini maoni yenu ya kujenga yatasikilizwa na hata kuzingatiwa.

Hitimisho 

Mheshimiwa Mufti, Waheshimiwa Masheikh, Waislamu Wenzangu na Wageni Waalikwa;

Nimesema sana na leo ni sikukuu sipendi kuwapunguzia muda wenu wa kwenda kusherehekea. Napenda kuwahakikishia kuwa Kiserikali tumejiandaa ipasavyo kulinda usalama wa mali na maisha ya wananchi katika kipindi chote cha sikukuu.

Mwisho kabisa nakushukuru tena, Mheshimiwa Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania kwa kunipa heshima hii kubwa. Nawatakia Waislam na Watanzania wote kwa jumla sikukuu ya Idd-El-Fitr yenye furaha na faraja tele. Nawaomba tuisherehekee kwa amani na salama. Eid Mubarak!!

Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania

Assalam Aleykum Warahmatullahi Taala, Wabarakatuh.

Asanteni Sana kwa kunisikiliza

No comments:

Post a Comment