HOTUBA YA WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO
UZINDUZI WA MRADI
USHIRIKI SAWA WA WANAUME WA KITANZANIA KWENYE AFYA YA UZAZI NA UJINSIA’
DAR ES SALAAM
6 SEPTEMBA 2011
Waziri wa Afya ,
Balozi wa Sweden Tanzania,
Mwakilishi Mkazi wa UNFPA
Katibu Mkuu wa RFSU,
Wanamtandao wa MenEngage,
Asasi za Kiraia
Wadau wa afya ya uzazi na jinsia
Wageni waalikwa, mabibi na mabwana
Ninayo furaha kubwa kuwa nanyi hapa asubuhi ya leo kufanya uzinduzi wa mradi wa uhamasishaji wa ushiriki wa wanaume kwenye afya ya uzazi na ujinsia mkoani Kitaifa.
Kwanza nianze kwa kuwashukuru wenzetu wa RFSU, shirika la Ki- Sweden linalojishughulisha na utoaji wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia, wanaondesha mradi huu kwa ubia na asasi za kiraia za RODI (Rukwa) na HAPA (Singida) kwa kuja na mradi huu muhimu wa oboreshaji wa afya ya uzazi na ujinsia.
Vilevile ningependa kuwashukuru shirika la misaada ya maendeleo la Sweden, Sida, kwa kufadhili mradi huu muhimu.
Pia niwashukuruni wageni waalikwa kwa kufika kwenu kwenye izinduzi rasmi wa mradi huu wa “ushiriki wa wanaume wa Kitanzania kwenye afya ya uzazi na ujinsia”. Karibuni sana.
Umuhimu wa ushiriki wa mwanaume kwenye afya ya uzazi na ujinsia
Ndugu wageni waalikwa,
Umuhimu wa ushiriki wa mwanaume kwenye kwenye afya ya uzazi na ujinsia ni mkubwa sana lakini kwa sababu za kimapokeo; mila na desturi, mambo yanayohusiana na uzazi yanaonekana kama ni ya wanawake tu. Na hii imechangia sana kufikia hali tuliyo nayo sasa ambapo tunashuhudia idadi kubwa ya vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi, idadi kubwa ya vifo vya watoto, kasi ya maambukizi ya magonjwa yaenezwayo kwa kujamiiana kama vile UKIMWI na mengineyo.
Ni kwa mapungufu haya ya ushiriki mdogo au kutoshiriki kabisa kwa mwanaume kwenye afya ya uzazi ndio RFSU na washirika wake RODI na HAPA wakaja na mradi huu wa kutoa elimu kwa jamii zetu za Kitanzania kuhusu umuhimu wa ushiriki kamili wa wanaume kwenye afya ya uzazi ili kuchangia kupunguza hali mbaya ya magonjwa na vifo ambavyo vyanzo vyake kwa namna moja ni mapungufu yaliyopo kwenye huduma ya afya ya uzazi na ujinsia, hasa ushiriki mdogo wa wanaume.
Ndugu wageni waalikwa,
Ushiriki wa mwanaume kwenye afya ya uzazi na ujinsia ambao mradi huu utashughulikia ni wa aina tatu;
Mosi, kwa mujibu wa mapokeo ya mila na desturi za jamii nyingi za kitanzania, mwanaume ndiye mmiliki na mtoa maamuzi juu ya matumizi ya rasilimali kuanzia kwenye kaya, jamii na hata katika ngazi ya kitaifa nafasi nyingi za utoaji maamuzi zinashikiliwa na akina baba. Hivyo kama wanaume hawatajua umuhimu wao wa ushiriki kwenye afya ya uzazi na ujinsia hata utoaji maamuzi juu ya kiasi cha rasilimali kinachotakiwa kutengwa kwa ajili ya afya ya uzazi katika family azao na jamii zao, hakitakidhi mahitaji.
Hivyo mradi huu kujishughulisha na uhamasishaji wa wanaume kwa ujumla wake juu ya umuhimu wa wao kushiriki kwenye afya ya uzazi utachangia kufanya mizania (balance) ya utoaji maamuzi kati ya wanawake na wanaume ambayo kwa namna moja au nyingine huathiri mfumo wa huduma za afya ya uzazi na ujinsia.
Pili, ushiriki wa wanaume kwenye utumiaji wa huduma za afya ni mdogo sana, hii ni kwa sababu ya desturi potofu kwamba anayezaa ni mwanamke hivyo kila kinachohusiana na uzazi ni cha mwanamke. Lakini ukweli ni kwamba hakuna mwanamke anayezaa bila mwanaume. Na hata baada ya mama kujifungua kazi ya ulezi ni jukumu la wazazi wote wawili. Hivyo mradi huu utajishughulisha pia na uhamasishaji wa wanaume kuzitumia huduma za afya ya uzazi na ujinsia zinazopatikana kwenye maeneo waliyomo. Kwanza ni haki yao kwa mujibu wa katiba ya nchi na itifaki mbalimbali za kimataifa ambazo serikali yetu ya Tanzania imeridhia, lakini pia inafaida kubwa sana kwa ustawi wa familia husika.
Tatu, ushiriki wa wanaume kama wahamasishaji; hii inalenga kuwafanya wanaume wawe wahamasishaji wa wanaume wengine kuwa washiriki wa afya ya uzazi na unjinsia kama nilivyotaja hapo mwanzo. Mradi utafanya kazi ya kuwahamasisha wanaume ili wakafanye kazi ya kuwahamasisha wanaume wenzao juu ya umuhimu wa wao (wanaume) kushiriki kwenye afya ya uzazi. Wanaume wengi wakisha hamasika wao pia wataweza kuwahamasisha hata akina mama kuhusu matumizi sahihi ya huduma za afya ya uzazi na ujinsia katika maeneo wanamoishi.
Pia mradi umenuia kuwahamasisha wanaume kushiriki katika utoaji huduma wa afya ya uzazi. Hivyo utafanya jitihada za kufanya uraghbishi (advocacy) ili mitaala ya mafunzo ya watoa huduma za afya ya uzazi isisitize ushiriki wa wanaume kwenye utoaji huduma ili tuweze kuongeza idadi ya wanaume watoa huduma za afya ya uzazi, na isionekane kuwa tasnia ya huduma za afya ya uzazi na ujinsia ni ya wanawake peke yao.
Ndugu wageni waalikwa,
Tunaamini tukifanikisha kuwashirikisha wanaume katika maeneo haya manne tutaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha afya ya uzazi na ujinsia hali ambayo itachangia kupunguza magonjwa na vifo vitokanavyo na mapungufu yaliyomo kwenye mfumo wa huduma za afya ya uzazi na ujinsia.
Nimefahamishwa kwamba mradi huu unafanyika kwenye mikoa miwili; Rukwa na Singida, (wilaya 3 kwa kila mkoa, jumla wilaya sita Tanzania) kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyoko kwenye mikoa husika, RODI (Rukwa) na HAPA (Singida). Moja ya kigezo kilichotumika kuchagua mikoa hii miwili ni hali ya kuwa pembezoni, si tu kijiografia lakini pia kihuduma. Hivyo ni matumaini yangu kwamba mradi huu utapata miongozo, ushauri na ushirikiano mzuri kutoka kwa halmashauri husika, taasisi za kiraia na wadau wa afya ya uzazi na ujinsia katika mikoa na wilaya hizi, ili tuweze kuchangia juhudi ya serikali ya kuimarisha afya na ustawi wa jamii zetu za kitanzania.
Ndugu wageni waalikwa mabibi na mabwana. Ninaomba ushirikiano wenu katika utekelezaji wa mradi huu muhimu.
Na sasa natamka rasmi kwamba mradi huu wa TMEP umezinduliwa rasmi
Asanteni sana
No comments:
Post a Comment