Wednesday, 22 June 2011

Wananchi waaswa kushiriki kikamilifu tamasha la Jinsia


‘Tamasha la jinsia
kufanyika mwaka huu Dar’

 Na Nasser Kigwangallah

MTANDAO wa mashirika watetezi wa haki za binadamu, usawa wa kijinsia na ukombozi wa wanawake nchini Tanzania (FemAct), wakishirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) wametangaza kuwa Tamasha la Jinsia la Mwaka 2011  litafanyika rasmi kuanzia tarehe 13 hadi 16 Septemba 2011.

Tamasha hilo litakuwa na mada kuu ‘Ardhi, Nguvu Kazi na  Maisha Endelevu’ ndani ya mada pana ya Jinsia, Demokrasia na Maisha Endelevu.

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) ni shirika la kiraia na kiuanaharakati, linalotetea mabadiliko ya kijamii kwa mtazamo wa kifeministi, ambayo yanalenga kwenye usawa wa jinsia, ukombozi wa wanawake, haki za kijamii, kufikia na kumiliki rasilimali kwa wanawake, vijana na makundi mengine yaliyoko pembezoni.

Dhana ya TGNP ni kujenga tapo la mabadiliko katika jamii, ambalo litachangia kuwepo kwa jamii yenye mabadiliko, ambayo inatambua na kuthamini masuala ya jinsia, demokrasia, haki za binadamu na haki za kijamii.

Mtandao wa Mashirika Watetezi wa Haki za Binadamu na Usawa wa Jinsia (FemAct) unajumuisha mashirika ya kiraia takribani 40 ambayo yamekuwa yakifanya kazi kupigania haki za kijamii ndani na nje ya Tanzania, tangu mwaka 1996.

Mtandao huu unalenga katika kuendeleza, kupanga mikakati na kutekeleza kwa pamoja ajenda za uanaharakati kwa ajili ya mabadiliko yanayozingatia haki za binadamu, usawa wa jinsia na demokrasia shirikishi, kiuchumi, kijamii, kisera na kiutendaji.

Tamasha la Jinsia 2011, litaandaliwa kwa kutumia mbinu za uraghbishi zilizokita katika katika harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi moja kwa moja.

Kwa kufanya hivi tunatarajia kuongeza umiliki ba ubunifu wa washiriki kwenye uendeshaji wa jukwaa la Tamasha.

Mada kuu, za jopo na za warsha zimetokana na ushiriki wa wadau pamoja na wanaharakati mbali mbali kuanzia ngazi ya jamii mpaka bara la Afrika na zaidi.

Tamasha la Jinsia kwa maana hiyo itakuwa jukwaa la wazi la kubadilishana uzoefu, kutoka ngazi zote, kuhusu mapambano ya ukombozi wa wanawake kimapinduzi.

Mada ya mwaka 2011 – ‘Ardhi, Nguvu Kazi na Maisha Endelevu’ inajengea kwenye mada zilizoongoza Tamasha za awali, na wakati huo huo inajengea kwenye kampeni kubwa ya ‘Haki ya Uchumi: Rasilimali ziwanufaishe wanawake walioko pembezoni.’

Tamasha la mwaka huu linalenga kuibua zaidi mapambano ya wanaharakati wanajamii wanawake, vikundi vyao na mitandao, kwenye masuala ya Archi, Nguvu Kazi na Maisha Endelevu ndani ya muktadha wa mfumo dume, sera za kibeberu na mifumo ya utandawazi.

Harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi iko mstari wa
mbele kwenye mapambano haya, kwa sababu ni wanawake walioko pembezoni ambao wananyonywa na kukandamizwa zaidi kwenye muktadtha huu.

Malengo ya tamasha la mwaka huu ni kuibua, kubadilishana, na kuanzisha fikra, uchambuzi na kutengeneza mikakati ya pamoja ya kudai rasilimali ziwanufaishe wanawake walioko pembezoni, kusherekea nguvu za wanawake kwa pamoja, kupanua na kuimarisha ushirikiano katika tapo la ukombozi wa wanawake kimapinduzi na haki ya uchumi katika ngazi na sekta zote za kijamii.

Malengo mengine ni kuimarisha, kujinoa na kuongeza uwezo wa kuchambua, kutafiti na kutathmini masuala yahusuyo haki za binadamu na za kijamii, usawa wa kijinsia na harakati za ukombozi wa wanawake na wanyonge wengine kote duniani.

Kuandika nyaraka na kusambaza maarifa kuhusu harakati za ukombozi wa wanawake duniani na kuchangia kwenye mjadala wa mada kuu ya Tamasha la Jinsia 2011.

Wanaharakati katika ngazi ya jamii, vikundi vya wanawake na wanaharakati wa haki za binadamu, demokrasia na ukombozi wa wanawake kimapinduzi, taasisi za kiraia na mitandao wanahamasishwa kutumia fursa ya tamasha la jinsia kuandaa mada na mawasilisho mbalimbali kwa kutumia sanaa, nyimbo, mashairi, mijadala, visa mikasa na maigizo kwenye warsha au jopo kuu.

Watumie fursa hiyo pia kufanya maonesho ya vitabu, picha, kazi za mikono kwa kuzingatia mada za Tamasha la Jinsia 2011. 

TGNP na FemAct wanahimiza pia utumiaji wa uwasilishaji kwa njia ya sanaa.

Ukombozi wa wanawake kimapinduzi unahusu mapambano dhidi ya mfumo dume,  ubeberu na ubepari na jitihada za wanawake na wasichana za kutengeneza mahusiano mbadala ya kijinsia ambapo wanawake na wanaume wataweza kutimiza ndoto zao na kufikia vilele vya uwezo wao. 
Ukombozi wa wanawake kimapinduzi unaunganisha mapambano ya wanawake na wanaume dhidi ya aina zote za ubaguzi, unyonyaji, na ukandamizaji, ikiwemo ubaguzi wa rangi, kijinsia, kitabaka, kikabila na
Kiutamaduni.

Pia kupambana na ubaguzi wowote unaotokana na hali ya kuishi na VVU, umri, kuishi na ulemavu, ujinsia n.k.

Ukombozi wa wanawake kimapinduzi unaamini kwamba mabadiliko yanawezekana, na hii amani inawapa moyo kwa kuwatoa katika hali ya kukata tamaa.

 Msimamo huu unasisitiza umuhimu wa nadharia na vitendo, uchambuzi na matendo.

Wakombozi wa wanawake kimapinduzi wanasisitiza umuhimu wa kutafakari kwenye uzoefu katika ngazi binafsi, pamoja na kwenye mapambano katika ngazi ya umma na umuhimu wa utafiti na uchambuzi wa kina kuhusu mifumo na mapambano.

Wanaharakati wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi wanatumia mbinu shirikishi katika michakato yote ya harakati katika kupinga ushindani wa kupindukia unaoongoza mfumo wa kibepari.

Njia mbadala za kujenga nguvu za pamoja, kuzalisha maarifa na mawasiliano zimejengwa ili kusaidiana na kulea kizazi za kuendeleza harakati hizi katika nadharia na vitendo.

Jopo la wazi litafanyika kila siku asubuhi kutoa muktadha utakao endesha mijadala ya siku hiyo.
...............................................................................................................................
0713 630 190/0784 630 195

No comments:

Post a Comment