Tuesday 14 June 2011

KILIMO NI UTI WA MGONGO


‘Kilimo Kwanza: Serikali itenge
bajeti ya kutosha kwa ajili ya kilimo’

Na Nasser Kigwangallah

BARAZA la Taifa la Biashara (TNBC) lilifanya mkutano wake tarehe 2 na 3 Juni, 2009 jijini Dar es Salaam, kujadili sera na mikakati ya kuleta mapinduzi ya kilimo cha Tanzania pamoja na utekelezaji wake chini ya kaulimbiu ya “Kilimo Kwanza.”
Hatua hii ilichukuliwa kwa kutambua ukweli kwamba asilimia themanini ya Watanzania wote hutegemea kilimo kwa ajili ya kuendeleza maisha yao.
Na kwa kutambua kuwa changamoto kubwa kwa Tanzania ni kupambana na umaskini na kwamba hili litawezekana tu kwa kuongeza tija katika kilimo.
Tanzania imejaaliwa kuwa na rasilimali nyingi na za kutosha kwa ajili ya mazao, mifugo na uvuvi; ambazo kwa sasa matumizi yake yapo chini sana.
Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kuwa na kiasi kikubwa cha maji kinachoweza kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji pamoja na ufugaji.
Ingawa jitihada nyingi na za makusudi zimekuwa zikichukuliwa ili kuboresha kilimo, lakini jitihada hizo hazijaweza kuleta mafanikio yoyote ya kuridhisha kuondoa balaa la njaa na umaskini kwa mkulima huko vijijini.
Ili kukuza kipato cha mkulima na kuweza kuondoa njaa hapa Tanzania, Kilimo iwe ndiyo dhana ya kuleta mapinduzi ya kijani kwa lengo la kukifanya kilimo cha Tanzania kuwa cha kisasa na cha kibiashara.
 Hivyo basi, dhana ya Kilimo Kwanza lazima ijumuishwe kwenye mipango mbalimbali ya Serikali ili kuhakikisha kwamba kunakuwa na mafanikio ya utekelezaji wake.
Serikali kwa upande wake, ifanye jitihada katika kuongeza rasilimali mbalimbali ili kufanikisha utekelezaji wa suala hili.
Na hii itawezekana tu ikiwa sekta binafsi itahamasishwa kikamilifu kuongeza uwekezaji kulingana na wajibu wake katika utekelezaji wa Kilimo Kwanza.
Hata hivo sera hiyo ya Kilimo Kwanza imekosolewa vikali na wanaharakati wa masuala ya kijinsia kuwa hakuna maslahi yeyote kwa wazalishaji wadogo wadogo, hasa wanawake walio pembezoni ambao wamesahaulika kabisa kwenye mpango mzima.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa Kilimo Kwanza kwa mtazamo wa Kijinsia katika makao makuu ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) hivi karibuni; Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Aida Isinika alisema ingawa juhudi za serikali za kuwainua kiuchumi wakulima kupitia mpango wa Kilimo Kwanza umeiwezesha Tanzania kuwa moja kati ya nchi zinazofaidika na Programu Mahususi ya Maendeleo ya Kilimo barani Afrika (CAADP), hakuna maslahi yeyote kwa wazalishaji wadogo wadogo, hasa wanawake walio pembezoni.
“Kilimo Kwanza hakina budi kuwaendeleza wakulima wadogo wadogo, hasa wanawake ili kupambana na umasikini na kuwainua kiuchumi ipasavyo,” anasema.
Anaongeza kusema kuwa Tanzania haijafikia viwango vinavyohitajika katika kuinua pato la mkulima na kama kweli tunataka kufaidika na mpango wa Kilimo Kwanza, sera hii iwanufaishe wakulima wadogo huko vijijini.
"Nchi zinazokubaliwa kusaini mkataba wa namna hii na CAADP ni zile ambazo serikali zake zinatenga zaidi ya asilimia sita ya bajeti yake kuchangia kilimo,” anasema.
Lakini serikali yetu kwa sasa inatenga asilimia nne tu ya bajeti yake katika kilimo, jambo ambalo bado halijaweza kufanikisha kuondoa njaa na umaskini hapa nchini.
Pia mpango wa kuwakaribisha wawekezaji kutoka nje kuja nchini utakuwa na mnufaa tu iwapo wawekezaji hao watashirikiana na wazalendo katika kukuza kilmo hapa nchini.
Pamoja na sera ya kilimo kwanza kuonekana kama njia sahihi ya kujenga uchumi wa Tanzania, hasa katika kipindi hiki cha mtikisiko wa uchumi duniani, pia inaonekana kama mkombozi wa maisha ya wananchi ambao asilimia 80 ni wakulima wadogo wanaoishi vijijini.
“Ili kuutoa uchumi wetu kutoka kwenye uchumi ulio nyuma na tegemezi na kuuingiza kwenye uchumi imara, wa kisasa na endelevu tunahitaji kufanya mapinduzi ya kweli katika sekta ya kilimo na viwanda,” anasema Profesa Isinika.
Mapinduzi haya yataongeza uzalishaji na tija na hivyo kuongeza ukuaji wa uchumi wetu.
Anafafanua kusema kuwa uzalishaji wa mazao ya kilimo ukiongezeka, mavuno yataongezeka na hivyo ongezeko hilo litawawezesha wakulima kunufaika kupata kipato kutokana na kuuza mazao mengi zaidi hapa nchini na nje pia.
Hii pia, inavutia wawekezaji kujenga viwanda vya usindikaji na utengenezaji wa bidhaa za viwandani kutokana na mazao ya kilimo.
Kwa hakika tukifanya mapinduzi hayo, tutakuwa tumetekeleza msemo uliozoeleka wa ‘maisha bora kwa kila Mtanzania.’
Lakini hata hivyo, pamoja na kaulimbiu hiyo, bado bajeti haijaonyesha waziwazi kuwa inatoa kipaumbele cha kwanza katika kilimo.
Kwa kuangalia katika mgawanyo wa mapato, sekta ya elimu bado inaongoza katika kutengewa kiasi kikubwa zaidi cha fedha (shilingi bilioni 1,743.9), ikifuatiwa na sekta ya miundombinu (shilingi bilioni 1,096.6), sekta ya afya (shilingi bilioni 963.0) halafu sekta ya kilimo (shilingi bilioni 666.9).
Kulingana na mgawanyo wa kisekta hapo juu, inaonyesha kuwa kaulimbiu hiyo haijakwenda sambamba na dhamira ya serikali ya kutoa kipaumbele cha kwanza katika kilimo.
Akizungumza hivi karibuni, Halima Mdee (Mbunge wa CHADEMA-Kawe), alisema kuna fedha chache tu za maendeleo ambazo zimetengwa katika sekta ya kilimo.
“Kati ya bajeti nzima ya fedha za maendeleo katika sekta hiyo, ni shilingi bilioni 23 tu zitatokana na fedha za ndani. Nyingine zinategemea fedha za wafadhili kutoka nje,”anasema.
Ikiwa hali ndiyo hiyo, basi hii ni fedheha dhahiri shahiri kwa ukuaji wa kilimo hapa nchini.
Mdee anaonyesha wasiwasi kuwa utegemezi huo hautaleta mafanikio katika sera ya kilimo kwanza kwani asilimia 70 ya fedha za wafadhili, ama haziji au zinachelewa kufika katika muda unaohitajika.
Mbali na wasiwasi huo, kuna masuala mbalimbali yanayojitokeza ambayo yanaonyesha uwezekano mdogo wa kutekeleza kivitendo sera hiyo.
Pamoja na serikali kuhimiza watu walime, bado kuna tatizo la miundombinu ya kupeleka bidhaa za kilimo katika masoko kama vile barabara, bandari na kadhalika.
Vile vile kuna wasiwasi kama msisitizo katika kilimo bila kuwekeza katika umwagiliaji unaweza kuwa na tija kwa taifa.
" Nguvukazi tunayo, lakini maji hatuna. Wazo la umwagiliaji linaweza kuwa msaada mkubwa kwetu," anasema mbunge Simba Chawene alipokuwa akichangia hotuba bungeni hivi karibuni.
Kwa kuangalia historia, siyo mara ya kwanza kwa Tanzania kutoa kipaumbele katika sekta ya kilimo.
Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kutangaza waziwazi kuwa ili tuendelee tunahitaji vitu vinne–watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Tafsiri ya maneno haya ni kwamba nguvukazi na ardhi ni muhimu mno katika maendeleo ya kilimo nchini.
Serikali yake pia ilikwenda mbali zaidi na kuwa na sera ya "siasa ni kilimo".
Azimio la Iringa la mwaka 1972 lilihimiza masuala mbalimbali kuhusu kilimo.
Kaulimbiu kama "kilimo ni uti wa mgongo" na "nguvu kazi" hazikuishia tu katika nadharia, ila kivitendo na wananchi walihimizwa kuanzisha mashamba ya ushirika vijijini, matumizi ya mbolea na pia kilimo cha kisasa chenye tija.
Hata hivyo, kwa maoni yangu, sera ya sasa imekuja wakati ambapo dunia inakabiliwa na mitikisiko mitatu – mtikisiko wa uchumi, sekta za fedha na kuongezeka kwa bei ya vyakula duniani.
Matatizo hayo yamedhoofisha jitihada za mataifa mbalimbali yanayoendelea kufikia lengo la kwanza la Maendeleo ya Milenia la kupunguza nusu ya watu wanaokabiliwa na njaa duniani ifikapo mwaka 2015.
Hali hii imetabiriwa kusukumiza wananchi wengi zaidi katika mataifa yanayoendelea, hasa katika bara la Afrika kwenye umaskini uliokithiri.
Kulingana na Jukwaa la Uchumi Duniani, kuna haja ya kuweka msisitizo katika kuwawezesha wakulima wadogo wadogo ili kukabiliana na hali ya sasa.
"Jitihada za kutokomeza umaskini na njaa na kukuza uchumi wa Afrika zitakuwa hazina matunda kama mahitaji ya wakulima wadogo wadogo katika kanda yanapuuzwa.
‘‘Kuongeza uzalishaji wa wakulima hawa kunawezekana na ni jambo la msingi kwa usalama wa chakula kwa Afrika na ukuaji wa uchumi kwa ujumla,’’ anasema Profesa Isinika.
Wakulima wadogo katika bara zima la Afrika wanaogelea peke yao.
Mwanamke hana bima dhidi ya hali ya hewa isiyokuwa na uhakika, hapati ruzuku na hapati mkopo.
Kwa ujumla wakulima wadogo katika hapa Tanzania, na barani Afrika kwa ujumla ni wanawake.
"Wakulima ni watoto na wanawake ambao ni wazee, huwezi kuona kijana katika kilimo," anasema.
Hatuwezi kuleta mapinduzi namna hii, mapinduzi yoyote yale ni vita.
Azimio la Maputo la mwaka 2003, linatoa wito kwa viongozi wa Afrika kutenga asilimia 10 ya bajeti za mataifa yao katika sekta ya kilimo ifikapo mwaka 2008 kama sehemu ya jitihada zao za kufikia lengo la kwanza la Maendeleo ya Milenia–kupambana na umaskini na njaa.
Hata hivyo, hadi sasa ni mataifa machache tu ambayo yamefikia lengo hilo huku Tanzania ikiwa siyo miongoni mwa mataifa hayo.
Mataifa yaliyofikia shabaha hiyo ni pamoja na Burkina Faso, Cape Verde, Chad, Ethipia, Mali, Malawi, Niger na Rwanda.
Pamoja na Tanzania kusisitiza katika kilimo kwanza, takwimu zinaonyesha kuwa kilimo kimetengewa asilimia saba tu ya bajeti ya mwaka huu kama ilivyokuwa kwa bajeti ya mwaka jana, na hivyo kuendelea kuwa chini ya lengo la asilimia kumi lililokubaliwa na Umoja wa Afrika.
Kilimo ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya uchumi, hususan katika Afrika ambapo watu wengi wanategemea kilimo.
Fedha nyingi zaidi za ASDP (75%) zinaelekezwa katika Halmashauri. Kuna pengo katika utoaji fedha za ASDP (52.7% hadi 2008).
Je, wananchi wanashirikishwa kuandaa miradi ya DADP na je, taarifa za mapato na matumizi zinatanganzwa katika magazeti?

Kwa ujumla fursa wazalishaji wadogo kushiriki ardhi kwa kilimo kwanza ni finyu sana na watabaki ni watazamaji tu.
Mapendekezo kubadlili sheria ya ardhi No 5 ya 1999  kamwe hayatalinda haki na usalama wa wazalishaji wadogo.
Wananchi wengi hawajui undani wa sheria hizi na utekelezaji wake; na hivyo vijiji vingi vimejuta kukubalia mikataba na wawekezaji bila kutambua undani wa yale waliyoyawekea saini.
Asilimia kubwa ya wananchi walikuwa kwenye kilimo wakati mikakati ya kuboresha kilimo inafanyika.
Baada ya mapinduzi ya kijani watu wengi waliondolewa kwenye kilimo.
Sababu: walishindwa kulipa madeni, walishindwa kumudu ushindani, mashamba yao madogo yalimegwa zaidi kutokana na mila za urithi. Na matokeo yake waliamua kuuza mashamba hayo, na wengi kukimbilia mijini kubangaiza.
Hata hivyo, kundi la watu walioondolewa kwenye kilimo limeendelea kuwa maskini zaidi katika nchi nyingi duniani.
Wananchi wanayo haki kudai fursa ya kushiriki katika michakato ya mipango ya DADPs katika wilaya zao, na kuainisha fursa zilizopo kwao na kuzitumia.
Kuepuka kuingizwa katika vikwazo ambavyo havitawanufaisha wao bali wageni watakaochukua ardhi yao.
Jukumu la Serikali ni kutengeneza mazingira ya uwekezaji kuwasaidia wakulima wadogo, wakati na wakubwa na kuelekeza nguvu kuwashirikisha na kuwasaida wakulima wadogo kama wadau wakubwa katika kilimo.
Na pia itenge bajeti ya kutosha kwa ajili ya kilimo asilimia 10, na ipunguze utegemezi kutoka kwa wafadhili nje.
……………………………………………………………………………
0713 630 190/0784 630 195



1 comment: