Tuesday 30 August 2011

Ujumbe wa Eid el-Fitr kutoka kwa Balozi wa Marekani


30 Agosti, 2011

Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni muda ambao Waislamu duniani kote wanafunga, wanaswali na kufanya matendo mema. Aidha, ni wakati wa kutafakari na kuimarisha imani zao, kutenda mema, kuwasaidia wenye shida na kuwa na huruma. Kwa niaba ya Watu wa Marekani, ninapenda kuwatakia Waislamu wote wa Tanzania Eid el-Fitr njema. 
Sherehe hizi zinahitimisha kipindi cha mwezi mzima wa kujitafakari na kutukumbusha kuwa maadili ya Uislamu - wema, kujali wengine, kuhudumia jamii, ushirikiano na huruma ni amali ambazo sisi kama Wamarekani tunazithamini sana na ambazo kwa hakika zimechangia sana katika tamaduni nyingi duniani kote.
Kama alivyosema Rais Barack Obama hapo tarehe 11 Agosti mwaka huu katika hafla ya Iftar iliyofanyika katika Ikulu ya Marekani, wakati wote Uislamu umekuwa sehemu ya familia ya Marekani na kwa muda mrefu mamilioni ya Wamarekani Waislamu wamekuwa wakichangia katika kuimarisha nchi yetu katika nyanja zote za maisha.  
 Balozi wa kwanza Muislamu nchini Marekani ambaye alikuwa akitoka Tunisia alialikwa na Rais Thomas Jefferson, ambaye aliandaa chakula cha jioni kwa wageni wake wakati wa magharibi kwa sababu kipindi hicho kilikuwa ni cha Ramadhani - na kufanya tukio hilo kuwa Iftar ya kwanza kuandaliwa na Ikulu ya Marekani - hiyo ilikuwa zaidi ya miaka 200 iliyopita. 
Jengo la kumbukubu ya Rais Thomas Jefferson katika jengo la Bunge la Marekani kuna bango liitwalo “Maelewano ya Binadamu” ambalo linauenzi Uislamu kama mambo makuu yaliyowezesha ustaarabu wa Marekani, hususan katika nyanja ya fizikia.
Marekani na Tanzania zinachangia utajiri mkubwa wa kuwa na watu wa dini na makabila mbalimbali. Katika ziara zangu kutembelea maeneo mbalimbali ya nchi hii nzuri ya Tanzania nimepata heshima kubwa ya kutembelea Misikiti, kukutana na viongozi wa kidini na waumini wa Kiislamu ili kukuza urafiki na ushirikiano wetu. 
Wakati Ramadhani ikielekea ukingoni, tudumishe moyo huo wa kushirikiana na kusaidiana kama jamii moja ili watoto wetu, bila kujali wamezaliwa wapi na wanaabudu vipi waweze kupata fursa ya kuwa vile walivyopangiwa kuwa kwa jina la Mwenyezi Mungu, na katika kuimarisha utu wetu.
Eid Mubarak.

Alfonso E. Lenhardt ni Balozi wa Marekani katika Jamhuri ya Muungano waTanzania

No comments:

Post a Comment