Thursday, 4 August 2011

Bunge huko Dodoma laigomea bajeti ya Wizara ya Uchukuzi

Waziri wa Uchukuzi  Bwana Omar Nundu (juu) na Naibu wake Bwana Athuman Mfutakamba (chini)

WABUNGE wameiweka njia panda bajeti ya Wizara ya Uchukuzi, baada ya wote waliochangia jana kuipinga na kutaka iondolewe bungeni ili Serikali ikajipange upya kama ilivyokuwa kwa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.
Wakichangia bajeti hiyo kwa nyakati tofauti jana, wabunge hao bila kujali itikadi za vyama vyao, walizungumza kwa kutanguliza maslahi ya nchi huku wakitamka: "Siungi mkono hoja."Kiongozi wa Kambi ya Upinzani
Mbunge wa Hai ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliwataka wabunge wote kuungana na kuipinga bajeti hiyo.
“Tuweke itikadi za vyama vyetu pembeni, tuungane pamoja tusiiunge bajeti hii mkono, tunaambiwa wizara iliomba Sh500 bilioni,  imepewa Sh90bilioni tu zitafanya nini hizi fedha?” alihoji Mbowe. Mbowe alisema bajeti hiyo haina fedha za kutoka kufanya mambo ya msingi na pia haijaainisha sawasawa, mikakati ambayo inatakiwa ifanywe ili kuimarisha sekta ya usafirishaji.
“Leo hii kama waziri ni mcha Mungu, asimame hapa atueleze ni shirika gani lililopo chini ya wizara hii linafanya shughuli zake kwa ufanisi. Kwa nini Serikali isiwajibike, kwa sasa hivi wawekezaji wanatuona sisi wote ni majuha, CCM majuha, Chadema Majuha.., nyie wakati huo mnaendelea kujivua magamba,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Mara zote huwa nasema, tufike mahali tujue kuwa, sisi wanasiasa kuna vitu ambavyo hatuna uwezonavyo, tutafute wataalamu wake wavifanye.”

Watanzania hawatatuelewa tukiipitisha:
Akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Buchosa (CCM), Dk Charles Chizeba alitoa sababu sita za kutounga mkono bajeti hiyo. Alisema bajeti hiyo ina tatizo kubwa la kimuundo, mipango haihusishwi na wizara nyingine na mipango kutotekeleza kutokana na fedha kidogo.
“Watanzania hawatatuelewa tukipitisha bajeti hii, tumeweka fedha nyingi katika barabara ambazo hazitadumu kwani baada ya miaka mitatu tutaanza kuwabana mawaziri ya ujenzi kutokana na kuharibika. Tumechoka kusikia takwimu, kusikia takwimu, watu wanataka ndege angani, wanataka usafiri wa reli uimarishwe,” alisema Dk Chizeba.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema),  Zitto Kabwe alisema bajeti hiyo haina jipya, huku akifafanua kuwa ana barua iliyoandikwa na Waziri wa Wizara hiyo, Omary Nundu kwenda kwa Waziri Mkuu, akiomba kuongezwa kwa fedha katika bajeti yake kwa ajili ya  kuimarisha miundombinu ya reli ya kati.“Majibu hayakupatikana hivyo bajeti haitatusaidia kitu.
Ni vyema wabunge tukaipa Serikali muda ili kurekebisha bajeti na kuja na mikakati thabiti,” alisema Zitto.Zitto alihoji sababu za Serikali kutaka fedha kutoka Benki ya Dunia (WB) ili kumlipa mtaalamu wa kufanya utafiti elekezi wa mahitaji ya reli ya kati: “Hivi mpaka leo hatujui mahitaji ya reli ya kati, wakati reli hii ipo tangu mwaka 1905?”“Tuisimamie nchi yetu, haiwezekani tupitishe bajeti ndogo kiasi hiki, mkipitisha bajeti hii mtakuwa hamjawatendea haki wananchi wa Kigoma na Tabora,” alisema Zitto.

No comments:

Post a Comment