Mwenyekiti wa kikao cha kujadili hatima ya mgawo nchini Bwana Malima Bundara, ambaye pia ni raisi wa Chama cha Wahandisi Tanzania (IET) akizungumza na wadau kwenye Ukumbi wa Karimjee jijini, Dar es Salaam siku ya Jumamosi. Picha: Na Nasser Kigwangallah
KATIKA harakati za kutatua mgawo wa umeme unaoendelea kote nchini,wahandisi jijini Dar es Salaam wameamua kuunda 'Kamati ya watu sita' kuisaidia serikali kuondokana na mgawo wa umeme unaoikumba Tanzania hivi sasa.
Raisi wa Taasisi ya Wahandisi nchini, Institution of Engineers Tanzania (IET) Injinia Malima Bundara aliwaambia waandishi wa habari Jumamosi jijini Dar es Salaam kuwa taasisi yake imeamua kuunda kamati kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalamu ili kuona tatizo hasa ni nini na kupendekeza njia muafaka ya kutatua tatizo hilo lisiweze kujirudia rudia mara kwa mara.
Hatua hiyo ilifikiwa juzi katika mkutano ulioitishwa na taasisi hiyo kujadil, kwa undani tatizo la umeme; mada kuu ikiwa ni “Ufumbuzi wa Kihandisi katika kutatua tatizo la umeme nchini Tanzania.”
Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam.
Akifanya majumuisho, mwenyekiti wa kikao hicho, yeye pia ni raisi wa taasisi hiyo, Dk. Malima Bundara, alisema kamati hiyo itaundwa na watu sita, watatu ni wahandisi kutoka taasisi yake na watatu kutoka serikalini.
Alizitaja wizara hizo kuwa ni pamoja na ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO).
Kwa mujibu wa Dk. Bundara, mapendekezo yatakayotolewa na kamati hiyo ambayo itafanya kazi ndani ya mwezi mmoja, yataweza kupelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete.
Alisema lengo la IET ni kuona tatizo la umeme linaondoka katika nchi hii hadi kufika mwishoni mwa mwaka huu, kwani wao kama wahandisi hawawezi kuacha suala hili lifanywe na wanasiasa na serikali peke yake.
Awali akichangia mada, mmoja wa wajumbe, Injinia Ibrahim Mwita, alisema tatizo la umeme limekuzwa na wahandisi wa TANESCO.
Kutokana na hali hii alisema ipo haja wahandisi hao kujikomboa wenyewe badala ya kusubiri mashinikizo kutoka kwa viongozi wao.
Kwa upande wake aliyewahi kuwa Rais wa taasisi hiyo, Injinia Kabyemera Julius, aliwataka wadau wengine watakaokuwa na maoni kufikisha maoni yao katika ofisi zao.
Pia Injinia Julius alisema tatizo lililopo serikalini kwa sasa ni kutokutoa taarifa kwa wananchi ambapo pale inapotokea mtu ana maoni yake inakuwa vigumu kujua aanzie wapi.
Katika hilo, alipendekeza kupata taarifa hizo kwa wakati na ikiwezekana serikali kuwaruhusu kwenda kutembelea vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme ili kuangalia kama kweli kinachoongelewa kinafanya kazi.
No comments:
Post a Comment