·
HOTUBA YA MGENI RASMI
·
KATIKA UFUNGUZI, MKUTANO WA WADAU WA URATIBU WA MAWASILIANO
YA VIRUSI VYA UKIMWI NA UKIMWI, KIROMO HOTEL
– BAGAMOYO: 29 AUGUSTI 2013
·
·
Mwenyekiti wa Mkutano
·
Mkurugenzi wa Uraghibishaji kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI
(TACAIDS)
·
Waratibu wa UKIMWI wa mikoa na manispaa mliopo hapa
·
Wadau wetu katika mapambano dhidi ya UKIMWI nchini
·
Wawakilishi kutoka asasi zisizo za kiserikali
·
Watekelezaji wa afua za mawasiliano ya VVU na UKIMWI
·
Wageni Waalikwa,
·
Mabibi na mabwana,
·
·
Ndugu Washiriki,
·
Kama ilivyo ada, nianze kwa
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa. Pia, nachukua fursa
hii, kwa niaba ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwakaribisha wote katika
mkutano huu wa uratibu wa mawasiliano ya VVU na UKIMWI. Kuwepo kwenu hapa
kunadhihirisha ni jinsi gani mlivyo mstari wa mbele katika vita dhidi ya adui
UKIMWI ambaye hivi sasa ana miongo
mitatu tangu aikumbe nchi yetu. Uwepo wenu pia, unaashiria kujitoa kwenu katika
kuhakikisha kwamba, mawasiliano ya VVU na UKIMWI nchini yanaboreshwa na kuwa
madhubuti katika kuzitangaza huduma za kinga ya VVU na zile za matunzo na
matibabu ya UKIMWI. Kwa mara nyingine, nawashukuru wote kwa utayari wenu wa
kushiriki mkutano huu.
·
·
Ndugu Washiriki,
·
Kama
mnavyofahamu, janga la UKIMWI linaendelea kuathiri sekta zote nchini. Sekta ya
afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya UKIMWI
nchini, imekuwa ikichukua juhudi za makusudi katika kudhibiti tangu janga hili
lilipoikumba nchi yenu mwanzoni mwa miaka ya 1980. Tangu kuanza kwa mapambano
dhidi ya UKIMWI nchini, wadau wengi wamekuwa
wakijishughulisha na kutekeleza
shughuli mbalimbali zinazolenga kutoa habari, elimu na mawasiliano dhidi ya VVU
na UKIMWI kwa jamii ya Tanzania ili kupunguza maambukizi mapya.
·
·
Kwa
kipindi chote hiki cha miongo mitatu ya
kuwepo kwa janga la UKIMWI nchini, sekta ya afya imekuwa ikijidhatiti katika
kuhamasisha Jamii kuhusu janga hili na kutoa huduma za ama kuzuia maambukizi au
kutoa huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU.
·
·
·
·
Ndugu Washiriki,
·
Kiwango
cha uelewa kuhusu VVU na UKIMWI miongoni mwa watanzania kimeongezeka kutoka
asilimia 5.7 mwanzo mwa miaka ya 1980 na kufikia zaidi ya asilimia 90 katika
miaka ya hivi karibuni. Pamoja na afua zingine, mafanikio haya yamefikiwa
kutokana na afua ya habari, elimu na mawasiliano, afua ambayo imekuwa
ikitekelezwa na wadau mbalimbali kwa kipindi chote hiki cha mapambano dhidi ya
UKIMWI nchini. Afua za mawasiliano zinazolenga makundi maalumu yaliyo katika
hatari zaidi ya kuambukizwa VVU, bila shaka zimechangia kwa kiasi kikubwa
mabadiliko ya tabia kwa watu walio katika makundi haya na matokeo yake ni
kupungua kwa kiwango cha maambukizi ya VVU. Kwa upande wake, Serikali ya
Tanzania ina shauku kubwa ya kuona kiwango cha maambukizi kinapungua hadi
kufikia sifuri. Hili linaweza kufikiwa pale tu sote kwa pamoja tutakapoboresha
juhudi zetu za sasa katika mapambano dhidi ya UKIMWI ikiwemo kuboresha afua ya
habari, elimu na mawasiliano.
·
·
Ndugu Washiriki,
·
Kadri
muda wa mapambano dhidi ya UKIMWI unavyosonga mbele, idadi ya wadau wanaojishughulisha na
mawasiliano ya VVU na UKIMWI wamekuwa wakiongezeka kwa kasi huku wakilenga
kuzitangaza afua mbalimbali za UKIMWI. Afua zenyewe ni kama vile damu salama,
udhibiti wa magonjwa ya ngono, ushauri nasaha na upimaji wa VVU, kuzuia
maambukizi ya VVU toka kwa mama kwenda kwa mtoto na huduma ya tohara kwa
wanaume. Kuzitangaza huduma hizi kunahitaji uwepo wa mfumo madhubuti wa utoaji
huduma husika ili kukidhi haja kama vile rasilimali watu. Kwa kuzingatia hayo,
sekta ya afya imeona kuna kila sababu ya kuratibu shughuli zetu za mawasiliano
hasa zile zinazolenga kutangaza huduma ambazo Wizara ina jukumu la kuzitoa.
Wizara inaamini kwamba, utaratibu huu kwa kiasi kikubwa utachangia uwajibikaji
miongoni mwa wadau mbalimbali kwani kabla ya kutangaza huduma. Mhusika atapaswa
kuwasiliana na Wizara kuona kama huduma zilizopo zinaweza kwenda sambamba na
ongezeko la wahitaji wa huduma husika.
·
·
Ndugu Washiriki,
·
Tarehe 27 Machi mwaka huu wa
2013, Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete
alizindua taarifa ya matokeo ya Utafiti wa Viashiria vya UKIMWI na Malaria ya
mwaka 2011/2012. Katika utafiti huo, imegundulika kwamba, asilimia 5.1 ya
Watanzania wenye umri wa kati ya miaka 15 na 49 wameambukizwa Virusi vya
UKIMWI. Kiwango hiki ni kidogo kwa asilimia 0.6 ukilinganisha na matokeo ya
utafiti wa mwaka 2007/2008 ambapo asilimia 5.7 ya Watanzania wenye umri kati ya
miaka 15 na 49 walikuwa wameambukizwa Virusi vya UKIMWI.
·
·
Ndugu Washiriki,
·
Kushuka
kwa kiwango cha maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa asilimia 0.6 tu kwa kipindi
cha takribani miaka minne ni kasi ndogo sana ya kuelekea kwenye azma yetu ya
Tanzania Bila UKIMWI Inawezekana. Ninaamini kwamba kuongeza kasi na ufanisi
katika shughuli zetu za elimu, habari na mawasiliano ni chachu katika kuchochea
kasi ya kushuka kwa kiwango cha maambukizi nchini. Ili tuwe na ufanisi, hatuna
budi kama wadau tuwe na uratibu mzuri wa kazi zetu na sio kila mdau kufanya
kivyake.
·
·
Ndugu Washiriki,
·
Kutokana
na kuwepo kwa wadau wengi wanaojishughulisha na mawasiliano ya VVU na UKIMWI,
watanzania wamekuwa wakipata taarifa hizo kutoka katika vyanzo mbalimbali.
Wingi wa vyanzo hivi unasababisha sekta ya afya kulazimika kutoa huduma za
ziada. Wakati mwingine, Serikali imekuwa ikilazimika kuongeza rasilimali ili
kununua vifaa husika na wakati mwingine kuweka juhudi ili kuhakikisha utolewaji
wa huduma za nyongeza ambazo zitaenda sambamba na ongezeko la watu.
·
·
Ndugu Washiriki,
·
Kutokana na
kutokuwa na uratibu mzuri wa kazi zetu za mawasiliano, Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI iliandaa Mkakati wa
Mawasiliano ya VVU na UKIMWI katika Sekta ya Afya. Mkakati huo unatekelezwa kwa
miaka nane, kuanzia 2008 hadi 2015. Mkakati huu uliandaliwa baada kufanyika upembuzi yakinifu katika
mikoa 8 ya Tanzania Bara na kubaini mapungufu katika mikakati yetu ya
Mawasiliano. Mikoa yenyewe ni pamoja na Arusha, D’Salaam, Dodoma, Iringa,
Kigoma, Mara, Mtwara na Shinyanga. Kwa kuzingatia mapungufu hayo, Mkakati
ulioandaliwa unatoa maelekezo ya jinsi ya kutatua mapungufu ya mawasiliano
yaliyobainishwa katika upembuzi yakinifu. Mkakati pia unatumika kama dira ya
kutekeleza mawasiliano yote yanayohusu VVU na UKIMWI katika sekta ya afya hasa
katika afua za kinga, tiba na matunzo, afua ambazo zinatekelezwa na wadau
mbalimbali nchini katika juhudi za kusaidia mapambano ya UKIMWI. Ni matumaini
yangu kwamba, wadau wote wanaojishughulisha na mawasiliano katika sekta ya afya
nchini watatumia mkakati huu katika kupanga, kutekeleza na hata kutathmini afua
za mawasiliano nchini.
·
·
·
Ndugu Washiriki,
·
Mkutano
huu wa siku mbili, unalenga kubadilishana uzoefu katika kutekeleza kazi za
mawasiliano ya VVU na UKIMWI, kazi ambazo zimekuwa zikitekelezwa kuanzia ngazi
ya taifa, mkoa, wilaya hadi jamii.
Mkutano huu pia unalenga kubadilishana uzoefu katika kuandaa mpango wa
utekelezaji wa mkakati wa mawasiliano ya VVU na UKIMWI katika sekta ya afya, na
kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa mkakati huo ambapo vipaumbele vya
ushirikishwaji miongoni mwa wadau na utekelezaji wake vimeainishwa.
·
·
Ndugu Washiriki,
·
Nadhani
sote tunafahamu kwamba, hivi sasa Dunia imedhamiria kufikia sifuri 3 ifikapo
mwaka 2015, yaani kuzuia maambukizi mapya ya VVU, vifo vinavyotokana na UKIMWI
na unyanyapaa. Ninashawishika kuamini kwamba afua ya mawasiliano ni suala
mtambuka ambapo litachangia kuifikisha Tanzania katika sifuri hizo 3.
Hatutaweza kuzuia maambukizi mapya endapo jamii haitapata taarifa sahihi za
jinsi ya kujikinga dhidi ya maambukizi. Pia, kutokomeza vifo vinavyotokana na
UKIMWI itakuwa ni ndoto endapo jamii haitapata taarifa sahihi jinsi ya
kutumia huduma za tiba na matunzo kwa
watu wanaoishi na VVU. Vilevile, kupiga vita unyanyapaa kunahitaji taarifa
sahihi ya njia za maambukizi ya VVU. Lakini haya yote yatafanikiwa pale tu sote kwa pamoja
tutakapokuwa na uratibu mzuri wa kazi zetu za mawasiliano hivyo, kuchochea
mabadiliko ya tabia miongoni mwa watanzania.
·
·
Ndugu Washiriki,
·
Tangu
kuanza kwa mapambano dhidi ya UKIMWI nchini, Serikali ya Marekani na Mfuko wa
Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria wamekuwa ni wafadhili wetu
wakubwa katika mapambano. Hivi karibuni, tumeshuhudia kupungua kwa raslimali
katika kutekekeleza mapambano dhidi ya UKIMWI nchini kutokana na ukweli kwamba
kuna baadhi ya wafadhili kama vile Serikali za Sweden na Denmark kujitoa. Kujitoa
kwa baadhi ya wafadhili hawa, kunamaanisha upungufu wa misaada pia. Hivyo,
ninatoa rai kwa wadau wa mawasiliano kutumia raslimali kwa ufanisi badala ya
kurudufu kazi miongoni mwa wadau zinazowalenga kundi lilelile la watanzania
hivyo kusababisha matumizi mabaya ya raslimali. Napenda kusisitiza kwamba, hili
nalo litafanikiwa endapo kila mdau atajua mwenzake yuko wapi, anafanya nini, na
kwa walengwa gani.
·
·
Ndugu Washiriki,
·
Yatupasa tutambue kwamba,
jukumu la kila mmoja wetu aliyehudhuria mkutano huu ni kueleza hali ya
utekelezaji wa afua za mawasiliano ya VVU na UKIMWI. Sote tuliopo hapa hatuna budi kushiriki kikamilifu katika
mkutano huu, kutoa uzoefu wetu katika mada husika ambao utasaidia kuboresha
mawasiliano ya VVU na UKIMWI nchini. Ninaamini kwamba, mkutano huu utakuwa na
tija kwetu kutokana na ukweli kwamba sote kwa pamoja bila kujali tofauti zetu,
tutakuwa na uelewa na kukubaliana kwa pamoja jinsi ya kuboresha kazi zetu
hivyo, kuongeza ufanisi katika kazi za mawasiliano tunazozifanya.
·
·
Ndugu Washiriki,
·
Kwa kumalizia hatuba yangu,
ninatoa pongezi kwa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa (CDC) kupitia asasi ya
Pathfinder kwa msaada wao ambao umetuwezesha
sote kukusanyika hapa na kupanga mikakati madhubuti katika kuendeleza mapambano
dhidi ya UKIMWI nchini. Msaada huu ni kiashiria tosha kuthibitisha ni jinsi
gani wadau wetu wa maendeleo wanavyofanya kazi bega kwa bega na serikali ili
hatimaye Tanzania nayo iweze kufikia lengo la milenia namba 6 la kupambana na UKIMWI, Malaria na magonjwa
mengine.
·
·
Mabibi na Mabwana,
·
Kwa heshima na taadhima,
nachukua fursa hii sasa kutangaza kwamba, mkutano wa uratibu wa mawasiliano ya
VVU na UKIMWI umefunguliwa rasmi.
·
·
Ahsanteni kwa Kunisikiliza
No comments:
Post a Comment