Sunday 1 September 2013

HOTUBA YA MGENI RASMI- Dr Anath Rwebembera, NACP acting Programme Manager

·         HOTUBA YA MGENI RASMI
·         KATIKA UFUNGUZI, MKUTANO WA WADAU WA URATIBU WA MAWASILIANO YA VIRUSI VYA UKIMWI NA UKIMWI, KIROMO HOTEL  – BAGAMOYO: 29 AUGUSTI 2013
·          
·         Mwenyekiti wa Mkutano
·         Mkurugenzi wa Uraghibishaji kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS)
·         Waratibu wa UKIMWI wa mikoa na manispaa mliopo hapa
·         Wadau wetu katika mapambano dhidi ya UKIMWI nchini
·         Wawakilishi kutoka asasi zisizo za kiserikali
·         Watekelezaji wa afua za mawasiliano ya VVU na UKIMWI
·         Wageni Waalikwa,
·         Mabibi na mabwana,
·          
·         Ndugu Washiriki,
·         Kama ilivyo ada, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa. Pia, nachukua fursa hii, kwa niaba ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwakaribisha wote katika mkutano huu wa uratibu wa mawasiliano ya VVU na UKIMWI. Kuwepo kwenu hapa kunadhihirisha ni jinsi gani mlivyo mstari wa mbele katika vita dhidi ya adui UKIMWI ambaye hivi sasa ana  miongo mitatu tangu aikumbe nchi yetu. Uwepo wenu pia, unaashiria kujitoa kwenu katika kuhakikisha kwamba, mawasiliano ya VVU na UKIMWI nchini yanaboreshwa na kuwa madhubuti katika kuzitangaza huduma za kinga ya VVU na zile za matunzo na matibabu ya UKIMWI. Kwa mara nyingine, nawashukuru wote kwa utayari wenu wa kushiriki mkutano huu.
·          
·         Ndugu Washiriki,
·         Kama mnavyofahamu, janga la UKIMWI linaendelea kuathiri sekta zote nchini. Sekta ya afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya UKIMWI nchini, imekuwa ikichukua juhudi za makusudi katika kudhibiti tangu janga hili lilipoikumba nchi yenu mwanzoni mwa miaka ya 1980. Tangu kuanza kwa mapambano dhidi ya UKIMWI nchini, wadau wengi wamekuwa  wakijishughulisha na  kutekeleza shughuli mbalimbali zinazolenga kutoa habari, elimu na mawasiliano dhidi ya VVU na UKIMWI kwa jamii ya Tanzania ili kupunguza maambukizi mapya.
·          
·         Kwa kipindi chote hiki cha  miongo mitatu ya kuwepo kwa janga la UKIMWI nchini, sekta ya afya imekuwa ikijidhatiti katika kuhamasisha Jamii kuhusu janga hili na kutoa huduma za ama kuzuia maambukizi au kutoa huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU.
·          
·          
·          
·         Ndugu Washiriki,
·         Kiwango cha uelewa kuhusu VVU na UKIMWI miongoni mwa watanzania kimeongezeka kutoka asilimia 5.7 mwanzo mwa miaka ya 1980 na kufikia zaidi ya asilimia 90 katika miaka ya hivi karibuni. Pamoja na afua zingine, mafanikio haya yamefikiwa kutokana na afua ya habari, elimu na mawasiliano, afua ambayo imekuwa ikitekelezwa na wadau mbalimbali kwa kipindi chote hiki cha mapambano dhidi ya UKIMWI nchini. Afua za mawasiliano zinazolenga makundi maalumu yaliyo katika hatari zaidi ya kuambukizwa VVU, bila shaka zimechangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya tabia kwa watu walio katika makundi haya na matokeo yake ni kupungua kwa kiwango cha maambukizi ya VVU. Kwa upande wake, Serikali ya Tanzania ina shauku kubwa ya kuona kiwango cha maambukizi kinapungua hadi kufikia sifuri. Hili linaweza kufikiwa pale tu sote kwa pamoja tutakapoboresha juhudi zetu za sasa katika mapambano dhidi ya UKIMWI ikiwemo kuboresha afua ya habari, elimu na mawasiliano. 
·          
·         Ndugu Washiriki,
·         Kadri muda wa mapambano dhidi ya UKIMWI unavyosonga mbele,  idadi ya wadau wanaojishughulisha na mawasiliano ya VVU na UKIMWI wamekuwa wakiongezeka kwa kasi huku wakilenga kuzitangaza afua mbalimbali za UKIMWI. Afua zenyewe ni kama vile damu salama, udhibiti wa magonjwa ya ngono, ushauri nasaha na upimaji wa VVU, kuzuia maambukizi ya VVU toka kwa mama kwenda kwa mtoto na huduma ya tohara kwa wanaume. Kuzitangaza huduma hizi kunahitaji uwepo wa mfumo madhubuti wa utoaji huduma husika ili kukidhi haja kama vile rasilimali watu. Kwa kuzingatia hayo, sekta ya afya imeona kuna kila sababu ya kuratibu shughuli zetu za mawasiliano hasa zile zinazolenga kutangaza huduma ambazo Wizara ina jukumu la kuzitoa. Wizara inaamini kwamba, utaratibu huu kwa kiasi kikubwa utachangia uwajibikaji miongoni mwa wadau mbalimbali kwani kabla ya kutangaza huduma. Mhusika atapaswa kuwasiliana na Wizara kuona kama huduma zilizopo zinaweza kwenda sambamba na ongezeko la wahitaji wa huduma  husika.
·          
·         Ndugu Washiriki,
·         Tarehe 27 Machi mwaka huu wa 2013, Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete alizindua taarifa ya matokeo ya Utafiti wa Viashiria vya UKIMWI na Malaria ya mwaka 2011/2012. Katika utafiti huo, imegundulika kwamba, asilimia 5.1 ya Watanzania wenye umri wa kati ya miaka 15 na 49 wameambukizwa Virusi vya UKIMWI. Kiwango hiki ni kidogo kwa asilimia 0.6 ukilinganisha na matokeo ya utafiti wa mwaka 2007/2008 ambapo asilimia 5.7 ya Watanzania wenye umri kati ya miaka 15 na 49 walikuwa wameambukizwa Virusi vya UKIMWI.
·          
·         Ndugu Washiriki,
·         Kushuka kwa kiwango cha maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa asilimia 0.6 tu kwa kipindi cha takribani miaka minne ni kasi ndogo sana ya kuelekea kwenye azma yetu ya Tanzania Bila UKIMWI Inawezekana. Ninaamini kwamba kuongeza kasi na ufanisi katika shughuli zetu za elimu, habari na mawasiliano ni chachu katika kuchochea kasi ya kushuka kwa kiwango cha maambukizi nchini. Ili tuwe na ufanisi, hatuna budi kama wadau tuwe na uratibu mzuri wa kazi zetu na sio kila mdau kufanya kivyake.
·          
·         Ndugu Washiriki,
·         Kutokana na kuwepo kwa wadau wengi wanaojishughulisha na mawasiliano ya VVU na UKIMWI, watanzania wamekuwa wakipata taarifa hizo kutoka katika vyanzo mbalimbali. Wingi wa vyanzo hivi unasababisha sekta ya afya kulazimika kutoa huduma za ziada. Wakati mwingine, Serikali imekuwa ikilazimika kuongeza rasilimali ili kununua vifaa husika na wakati mwingine kuweka juhudi ili kuhakikisha utolewaji wa huduma za nyongeza ambazo zitaenda sambamba na  ongezeko la watu.
·          
·         Ndugu Washiriki,
·         Kutokana na kutokuwa na uratibu mzuri wa kazi zetu za mawasiliano, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI iliandaa Mkakati wa Mawasiliano ya VVU na UKIMWI katika Sekta ya Afya. Mkakati huo unatekelezwa kwa miaka nane, kuanzia 2008 hadi 2015. Mkakati huu uliandaliwa  baada kufanyika upembuzi yakinifu katika mikoa 8 ya Tanzania Bara na kubaini mapungufu katika mikakati yetu ya Mawasiliano. Mikoa yenyewe ni pamoja na Arusha, D’Salaam, Dodoma, Iringa, Kigoma, Mara, Mtwara na Shinyanga. Kwa kuzingatia mapungufu hayo, Mkakati ulioandaliwa unatoa maelekezo ya jinsi ya kutatua mapungufu ya mawasiliano yaliyobainishwa katika upembuzi yakinifu. Mkakati pia unatumika kama dira ya kutekeleza mawasiliano yote yanayohusu VVU na UKIMWI katika sekta ya afya hasa katika afua za kinga, tiba na matunzo, afua ambazo zinatekelezwa na wadau mbalimbali nchini katika juhudi za kusaidia mapambano ya UKIMWI. Ni matumaini yangu kwamba, wadau wote wanaojishughulisha na mawasiliano katika sekta ya afya nchini watatumia mkakati huu katika kupanga, kutekeleza na hata kutathmini afua za mawasiliano nchini.
·          
·          
·         Ndugu Washiriki,
·         Mkutano huu wa siku mbili, unalenga kubadilishana uzoefu katika kutekeleza kazi za mawasiliano ya VVU na UKIMWI, kazi ambazo zimekuwa zikitekelezwa kuanzia ngazi ya taifa, mkoa, wilaya hadi jamii.  Mkutano huu pia unalenga kubadilishana uzoefu katika kuandaa mpango wa utekelezaji wa mkakati wa mawasiliano ya VVU na UKIMWI katika sekta ya afya, na kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa mkakati huo ambapo vipaumbele vya ushirikishwaji miongoni mwa wadau na utekelezaji wake vimeainishwa.
·          
·         Ndugu Washiriki,
·         Nadhani sote tunafahamu kwamba, hivi sasa Dunia imedhamiria kufikia sifuri 3 ifikapo mwaka 2015, yaani kuzuia maambukizi mapya ya VVU, vifo vinavyotokana na UKIMWI na unyanyapaa. Ninashawishika kuamini kwamba afua ya mawasiliano ni suala mtambuka ambapo litachangia kuifikisha Tanzania katika sifuri hizo 3. Hatutaweza kuzuia maambukizi mapya endapo jamii haitapata taarifa sahihi za jinsi ya kujikinga dhidi ya maambukizi. Pia, kutokomeza vifo vinavyotokana na UKIMWI itakuwa ni ndoto endapo jamii haitapata taarifa sahihi jinsi ya kutumia  huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU. Vilevile, kupiga vita unyanyapaa kunahitaji taarifa sahihi ya njia za maambukizi ya VVU. Lakini haya yote  yatafanikiwa pale tu sote kwa pamoja tutakapokuwa na uratibu mzuri wa kazi zetu za mawasiliano hivyo, kuchochea mabadiliko ya tabia miongoni mwa watanzania. 
·          
·         Ndugu Washiriki,
·         Tangu kuanza kwa mapambano dhidi ya UKIMWI nchini, Serikali ya Marekani na Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria wamekuwa ni wafadhili wetu wakubwa katika mapambano. Hivi karibuni, tumeshuhudia kupungua kwa raslimali katika kutekekeleza mapambano dhidi ya UKIMWI nchini kutokana na ukweli kwamba kuna baadhi ya wafadhili kama vile Serikali za Sweden na Denmark kujitoa. Kujitoa kwa baadhi ya wafadhili hawa, kunamaanisha upungufu wa misaada pia. Hivyo, ninatoa rai kwa wadau wa mawasiliano kutumia raslimali kwa ufanisi badala ya kurudufu kazi miongoni mwa wadau zinazowalenga kundi lilelile la watanzania hivyo kusababisha matumizi mabaya ya raslimali. Napenda kusisitiza kwamba, hili nalo litafanikiwa endapo kila mdau atajua mwenzake yuko wapi, anafanya nini, na kwa walengwa gani.  
·          
·         Ndugu Washiriki,
·         Yatupasa tutambue kwamba, jukumu la kila mmoja wetu aliyehudhuria mkutano huu ni kueleza hali ya utekelezaji wa afua za mawasiliano ya VVU na UKIMWI. Sote tuliopo hapa  hatuna budi kushiriki kikamilifu katika mkutano huu, kutoa uzoefu wetu katika mada husika ambao utasaidia kuboresha mawasiliano ya VVU na UKIMWI nchini. Ninaamini kwamba, mkutano huu utakuwa na tija kwetu kutokana na ukweli kwamba sote kwa pamoja bila kujali tofauti zetu, tutakuwa na uelewa na kukubaliana kwa pamoja jinsi ya kuboresha kazi zetu hivyo, kuongeza ufanisi katika kazi za mawasiliano tunazozifanya. 
·          
·         Ndugu Washiriki,
·         Kwa kumalizia hatuba yangu, ninatoa pongezi kwa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa (CDC) kupitia asasi ya Pathfinder kwa msaada wao ambao umetuwezesha  sote kukusanyika hapa na kupanga mikakati madhubuti katika kuendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI nchini. Msaada huu ni kiashiria tosha kuthibitisha ni jinsi gani wadau wetu wa maendeleo wanavyofanya kazi bega kwa bega na serikali ili hatimaye Tanzania nayo iweze kufikia lengo la milenia namba 6 la kupambana na UKIMWI, Malaria na magonjwa mengine.
·          
·         Mabibi na Mabwana,
·         Kwa heshima na taadhima, nachukua fursa hii sasa kutangaza kwamba, mkutano wa uratibu wa mawasiliano ya VVU na UKIMWI umefunguliwa rasmi.
·          
·         Ahsanteni kwa Kunisikiliza


No comments:

Post a Comment